RAIS wa Fountain Gate Academy, Japhet Makau, amesema uongozi unaridhishwa na mwenendo wa timu yao ya Fountain Gate FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara huku akisisitiza kwamba ipo katika njia sahihi.
Timu hiyo ambayo inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya kucheza mechi 11 imekusanya pointi 17, sambamba na kufunga mabao 20 na kuruhusu 20.
Makau ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma kwenye kikao cha kufanya tathmini kuhusu miradi mbalimbali iliyoko chini ya Fountain Gate Academy.
Amesema mpaka sasa wanaridhishwa na mwenendo wa timu hiyo japo kwenye upande wa ulinzi wameona kuna changamoto, hivyo wanasubiri kufunguliwa kwa dirisha dogo ili kufanya maboresha.
“Tumejiona tuna changamoto kwenye safu ya ulinzi ambapo tumekuwa tukifungwa sana mabao, kwa hiyo hilo ni eneo ambalo tutalichukulia hatua kubwa katika kipindi kijacho cha usajili cha dirisha dogo linalokuja ili kufanya marekebisho kuhakikisha tunafanya vizuri, malengo yetu ni kumaliza nafasi nne za juu katika ligi,” amesema Makau.
Mbali na hilo, Makau amesema mpaka sasa wamefanikiwa kuwapeleka wachezaji watatu nje ya nchi kwa ajili ya kucheza mpira kutoka kwenye Academy yao ikiwemo nchi za Hispania, Austria na Misri huku mipango ikiwa ni kuanzisha shule maalum jijini Mwanza kwa ajili ya kuinua vipaji kwa vijana itakayoitwa Youth Empowerment Through Soccer (YET).