Dar City walistahili NBL | Mwanaspoti

DAR city ndio mabingwa wa Ligi ya Kikapu ya Taifa (NBL) iliyomalizika katika viwanja vya CHinangali, Dodoma, lakini kama hujui kilichoipa ubingwa ni mambo mawili tu.

Dar City ilicheza fainali na ABC na kuifunga katika michezo miwili, wa kwanza ikishinda kwa pointi 97-46 na wa pili kwa 78-46 na kuwa ushindi wa 2-0.

Kilichoibeba timu hiyo ni usajili iliyofanya wa nyota wa kimataifa na uwepo wa benchi bora la ufundi chini ya Kocha Mohamed Mbwana.

Wachezaji wa kigeni waliosajiliwa ni Jshin Brownlee, Jamel Marbuary (Marekani) Gilbert Nijimbere (Burundi), Victor Mwoka na Bramweli Mwombe (Kenya).

Nyota hao wa kimataifa  walishirikiana vizuri na Mtanzania  aliyewahi kucheza ligi ya Marekani (NBA), Hasheem Thabeet, Amini Mkosa, Fotius Ngaiza, Stanley Mtunguja, Josephat Peter na Haji Mbegu.

Licha ya ABC kuonyeha ushindani lakini ubora wa nyota wa Dar City uliidhohofisha na katika robo ya  kwanza City iliongoza kwa pointi 25-11, 23-14, 11-11 na 19-10.

Timu zilizoshiriki upande wanaume ni Eagles (Mwanza) JKT (DSM), TBT (Kigoma), ABC (DSM) na Kihonda Heat (Morogoro).

Zingine ni Mvumi Rippers (Dodoma), Dar City (DSM), Kisasa Heroes (Dodoma) na Pamoja BC (Arusha).

Wachezaji  wanne wa Dar City na ABC walikuwa kivutio katika fainali hiyo ya pili ya ligi ya kikapu (NBL).

Wachezaji hao ni Brownlee, Nijimbere, Mkosa (Dar City) na Alinani Endrew kutokana na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi zao vizuri, pamoja na kuziwezesha  timu zao zikapata  ushindi.

Brownlee anayecheza namba mbili ‘shooting guard’, aliongoza kwa  kufunga katika maeneo ya mitupo mitatu ‘three points’ pamoja na maeneo ya mitupo miwili.

Mbali ya kufunga, katika mchezo huo alidanki mara sita na kufunga pointi 20.

Nijimbere ambaye ni raia wa Burundi,  nafasi anayocheza ni namba moja ‘point guard’ alikuwa ni kiungo kizuri cha kuchezesha timu yake na kutoa pasi za ‘assist’ pamoja na kufunga.

Katika mchezo huo alitoa ‘assist’ mara 12 na pointi alizofunga ni 12.

Mkosa  anayecheza namba 3 ‘small forward’, alionekana ni fundi wa kupokonya mipira ‘steal’, kutoa ‘assist’ na kufunga na alipokonya mipira mara nane, asisti tano na kufunga 10.

Endrew anayecheza namba moja ‘point guard’, alichangia timu yake kutoa ushindani kwa timu ya Dar City.

Nyota huyo  alikuwa kivutio eneo la katikati pindi wanapokabana na Nijimbere wa Dar City, katika mchezo huo alifunga point 10.

Related Posts