Simba, Yanga zatoa pole kifo cha Dk Ndugulile

Klabu za Simba n Yanga zimetoa pole kwa familia, ndugu, Bunge la Tanzania, jamaa na marafiki baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Kigamboni Dk Faustine Ndugulile kilichotokea leo Novemba 27, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu
Kwa kuonyesha masikitiko yao, klabu hizo zimetoa taarifa kwa umma zikiwa na ujumbe wa salamu za rambirambi. 

Taarifa ya klabu ya Simba ilisomeka: “Klabu ya Simba imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya – kanda ya Afrika, kilichotokea nchini India leo tarehe 27 Novemba 2024.

“Klabu yetu inatoa pole kwa Spika wa Bunge, Wanakigamboni, familia, ndugu, jamaa na marafiki.

“Tunasikitika kupoteza mwanachama na shabiki muadilifu wa klabu yetu. Tutaendelea kuenzi mchango wake katika ustawi wa klabu yetu.”

Enzi za uhai wake Dk Ngulile alionyesha wazi kuwa shabiki wa klabu ya Simba na alikuwa akiposti hata kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akishauri klabu na hata akionyesha kufurahishwa kipindi timu hiyo ikifanya vizuri na kuhuzunishwa pia inapofanya vibaya.

Taarifa ya klabu ya Yanga katika taarifa yake imesema: “Uongozi wa Klabu ya Young Africans Sports Club umepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Dkt.  Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la Afya Duniani [WHO]-Kanda ya Afrika, kilichotokea nchini India, usiku wa kuamkia leo, Novemba 27, 2024”.

“Kwa niaba ya Wanachama, Wapenzi na Mashabiki, Uongozi wa Young Africans Sports unatoa pole kwa Spika wa Bunge, Wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huu”.

“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi”.