MASHINDANO ya kikapu kwa timu za vijana yamezidi kushika kasi na Juhudi imeitambia Stone Town ya Zanzibar kwa pointi 20-9 kwenye viwanja vya Kituo cha Michezo cha JMK Youth Park.
Mchezo huo ulikuwa ni timu za vijana U16, huku pia ikipigwa michezo mingine ya Vijana U14 na mashindano hayo ya siku nne yajulikanano kama JMK Basketball Tournament yanashirikisha timu 50 kutoka Kenya, Tanzania Bara na Zanzibar.
Michezo mingine iliyochezwa ya U14, Milenium ya Zanzibar iliishinda Juhudi kwa pointi 24-7.
Kwa upande wa umri wa miaka 16, Juhudi pia iliinyoosha Orkeeswa kwa pointi 13-10.
Timu ya wasichana ya U14 ya Orkeeswa ya Arusha iliitambia Ukonga kwa pointi 15-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, kwenye viwanja hivyo, Mratibu wa Michezo wa kituo JMK Youth Park, Bahati Mgunda alisema mashindano hayo yanafanyika kila mwaka na kuzipongeza timu zote zilizoshiriki mashindano hayo, ikiwemo kutoka Kenya ambayo imeonyesha ushindani dhidi ya wenyeji.