Dodoma. Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu serikalini, watajifungia kwa siku tatu kujadili masuala mbalimbali ya watumishi wa umma ikiwemo namna ya kushughulikia malimbikizo na bajeti ya mishahara.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 12, 2024 wakati akizungumzia kuhusu kikao kazi hicho kitakachokaa kuanzia Desemba 17 hadi 19, mwaka huu.
Daudi amesema kikao hicho kinawashirikisha wakuu hao kutoka katika wizara, taasisi za umma na Serikali za mitaa.
Amesema katika kikao hicho, watabadilishana mawazo na maelekezo kuhusu vipaumbele vya Serikali kwenye ajira za watumishi wa umma pamoja na maandalizi ya ikama na bajeti ya mishahara.
“Malengo hasa ya kikao kazi hiki ni kubadilishana uzoefu, tunajua utumishi wa umma ni mpana sana na nchi yetu ni kubwa, wale wanaofanya vizuri wanaongea na wenzao na wanabadilishana zile changamoto ili tuwahudumie Watanzania vizuri,”amesema.
Amesema kikao hicho pia kitatumika kupeana maelekezo ili kazi za Serikali zifanyike vizuri kwenye maeneo yanayolegalega.
Naye, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ibrahim Mahumu, amesema maeneo mengine watakayojadili ni usimamizi wa rasilimaliwatu na namna ya kushughulikia malimbikizo ya mishahara.
“Tumeona kuna maeneo yana changamoto na tunaweza kuwashirikisha na kutengeneza njia bora ya kuweza kutatua changamoto kwa watumishi wetu walioko taasisi mbalimbali za Serikali,”amesema.
Mahumu amesema wanaelekea mwisho wa mwaka, kuna mambo mengi ya kuwekana sawa ili wanapoanza kubainisha mahitaji ya watumishi wanaopaswa kuajiriwa wawe wamepeana maeneo ya vipaumbele vya Serikali.
Amesema kwa kufanya hivyo watajua mahitaji yao na vipaumbele kuhusu aina ya watumishi wanaopaswa kuajiriwa kwa mwaka husika.