John Tendwa aacha alama ya ujasiri

Dodoma. Kifo cha John Tendwa, msajili mstaafu wa vyama vya siasa, kimeibua kumbukumbu mbalimbali za utendaji wake uliojaa mambo mengi, ukiwepo ujasiri.

Kwa mujibu wa mwanaye William, Tendwa aliyeitumikia ofisi ya msajili kwa miaka 13 amefariki dunia saa nane usiku wa kuamkia leo Desemba 17, 2024 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa MuhimbilI (MNH).

Mbali na namna tofauti wanavyomweleza wanasiasa waliokuwa wadau wa ofisi yake, kumbukumbu zilizozopo zinabainisha alikuwa msajili mwenye ujasiri wa kipekee, hakusita kukosoa hata viongozi wa Serikali na chama tawala cha CCM.

Msimamo wake wa kutetea demokrasia ulionekana kuwa na sura mbili, kwani licha ya kuonya kuhusu matumizi mabaya ya rasilimali za Serikali katika kampeni, bado wapinzani walimtuhumu kuwa na upendeleo kwa chama tawala.

Tendwa aliwahi kunukuliwa akisema kukua kwa demokrasia nchini kupitia mfumo wa vyama vingi kunaweza kuing’oa CCM madarakani.

Hata hivyo, kauli hizi hazikumfanya kuwa kipenzi cha upinzani, kwani mara kadhaa Chadema, CUF na TLP walimshutumu kwa kile walichokiita ‘muua demokrasia’. Katika kipindi chake kama msajili, aligongana na vyama hivi hasa alipotoa kauli za kutishia kufuta usajili wao kwa madai ya kuchochea vurugu.

Ujasiri kukosoa CCM, Serikali

Ujasiri wa Tendwa haukuwa tu wa kukosoa upinzani, mara kadhaa alitoa kauli za kuwakosoa viongozi wa CCM na Serikali pale alipohisi wamekwenda kinyume cha misingi ya demokrasia.

Alikosoa matumizi ya nyenzo za Ikulu, akisema si sahihi picha za Ikulu kutumika kwenye kampeni za uchaguzi kwa faida ya chama tawala.

Tendwa alionya kuwa picha hizo zinaonyesha wazi kuwa rasilimali za umma zinatumika kwa masilahi ya chama kimoja, jambo ambalo linapunguza usawa wa kisiasa.

Pia aliwakosoa viongozi wa juu serikalini, akiwemo Rais wa wakati huo Jakaya Kikwete. Alimlaumu kwa kutoa msimamo wa kuipinga rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Kwa mujibu wa Tendwa, Kikwete, kama kiongozi wa nchi, alipaswa kutoa mwongozo wa jinsi Bunge hilo linavyopaswa kufanya kazi badala ya kueleza upinzani wake waziwazi.

Ujasiri huu haukuishia Tanzania Bara pekee. Alikosoa viongozi wa Zanzibar akiwemo Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Pili wa SMZ, Balozi Seif Ali Iddi, kwa kutoa kauli zilizokinzana na demokrasia katika mikutano ya hadhara.

Kauli dhidi ya UVCCM, mfumo wa uchaguzi

Katika mojawapo ya matamshi yake, Tendwa aliwahi kusema CCM inawatumia vijana wa UVCCM kufanya vurugu dhidi ya vyama vingine vya siasa.

Aliyataja matukio ya kuchana mabango ya wapinzani na kuondoa bendera za vyama hivyo kama mifano ya vitendo vinavyokwamisha demokrasia nchini.

Kauli hizi zilimfanya kuonekana kama mpinzani wa CCM, ingawa kwa upande mwingine wapinzani walimshutumu kwa upendeleo.

Si hayo tu, Tendwa baada ya kustaafu alimkosoa pia msajili aliyemfuata, Jaji Francis Mutungi kuhusu ukomo wa madaraka ndani ya vyama vya siasa.

Alisema hakuna sheria inayolazimisha ukomo wa uongozi wa chama, bali ni jambo la kikatiba ndani ya vyama husika.

Hata hivyo, alisema wakati wake wa uongozi alipendekeza suala la ukomo wa viongozi liwekwe kwenye katiba za vyama vya siasa.

Kuna wakati, Tendwa aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa kina kwa wagombea wanaojitoa baada ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi.

Alisema vitendo hivyo vinatia shaka na kuashiria uwepo wa mazingira ya rushwa au shinikizo la kisiasa.

Midahalo ya wagombea urais

Moja ya mambo yaliyomfanya Tendwa kuwa tofauti na mtangulizi wake ni msimamo wake wa kuunga mkono midahalo ya wagombea wa urais.

Alisisitiza midahalo ni muhimu kwa wapigakura kuelewa sera za wagombea. Aliwahi kunukuliwa akisema: “Mimi kama msajili ninaunga mkono kuwepo kwa midahalo ya wagombea ili kila mmoja apate nafasi ya kueleza sera zake… bora utaratibu ukawekwa hata wakifanya midahalo ya wagombea wanne, siyo mbaya.”

Kauli hii ilionyesha msimamo wake thabiti wa kutaka usawa wa kisiasa na kuongeza uwazi katika uchaguzi.

Tendwa, ambaye ni wakili na aliwahi kuwa mwenyekiti wa Mahakama ya Kazi, alikumbana na changamoto nyingi katika nafasi yake ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Alisimulia namna alivyoanza kazi hiyo kwa changamoto kubwa baada ya mtangulizi wake, Jaji George Liundi kuamua kuwania ubunge wa Afrika Mashariki kupitia CCM.

Tendwa alieleza hatua ya Liundi ilimweka katika mazingira magumu, kwani watu walihisi kuwa hata yeye ni mwanachama wa CCM na kwamba angefuata nyayo za mtangulizi wake.

Hata hivyo, alikanusha madai hayo akisema:

“Mimi si mwanachama wa chama chochote. Mimi ni mshauri mtaalamu na msuluhishi wa migogoro ya kisiasa katika nchi mbalimbali za Afrika. Uamuzi wa mtangulizi wangu uliathiri mtazamo wa watu, lakini mimi nilifanya kazi yangu kwa weledi.”

Moja ya matukio ya kusisimua katika maisha ya kazi ya Tendwa ni lile la kufungiwa ndani ya ofisi za CUF Zanzibar.

Alisimulia kuwa mwaka 2001, alifungiwa ndani ya ofisi hizo huku milango na madirisha yakiwa yamefungwa, isipokuwa sehemu ndogo tu ya madirisha ya juu. Wafuasi wa CUF walimtuhumu kuwa yeye ni mtu wa CCM.

“Wakanifungia ndani, wakaniambia nisiseme chochote. Kwa zaidi ya saa mbili na nusu walizungumza wao, sikutakiwa kujibu chochote. Baada ya kumaliza, walinipa nafasi ya kuzungumza na nikatumia saa moja na nusu kueleza msimamo wangu. Tukio hilo lilinijengea heshima kwa CUF na walitambua kuwa mimi si mtu wa CCM kama walivyokuwa wanadhani.”

Baada ya kustaafu nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tendwa alianzisha kampuni ya uwakili, JB Advocates.

Alibaki kuwa mshauri wa masuala ya siasa na msuluhishi wa migogoro katika nchi za Afrika.

Katika mahojiano mbalimbali alionyesha kujivunia mchango wake katika kuimarisha demokrasia Tanzania licha ya changamoto alizokumbana nazo.

John Tendwa atakumbukwa kama kiongozi shupavu, mwenye msimamo usiotetereka katika masuala ya demokrasia na usawa wa kisiasa.

Alisimamia vyama vya siasa kwa haki, lakini ujasiri wake wa kusema anachokiamini mara nyingi ulimweka katika hali ya utata. Hata hivyo, mchango wake katika historia ya demokrasia nchini Tanzania hautasahaulika.

Mwisho wa safari yake, Tendwa anaacha alama isiyofutika katika siasa, hususani nafasi ya usajili wa vyama vya siasa, ambayo aliihudumia kwa uadilifu mkubwa.