Mwenyekiti mpya Chadema Kaskazini asema hatarithi maadui

Arusha. Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel amewaomba viongozi wa majimbo na mikoa katika kanda hiyo kushirikiana kuimarisha chama hicho huku akieleza kwamba hataki kurithi maadui.

Welwel ameshinda nafasi hiyo baada ya uchaguzi huo akirithi mikoba ya Godbless Lema ambaye amempongeza kwa ushindi huo na kuahidi kushirikiana naye katika kazi.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Desemba 19, 2024 jijini Arusha, upigaji kura ulirudiwa mara ya pili kwa nafasi ya mwenyekiti, baada ya wagombea watatu wa nafasi hiyo kushindwa kufikisha asilimia 50 ya kura zinazotakiwa kwa mujibu wa katiba.

Awali, Welwel alikuwa amepata asilimia 42, Michael Kilawila asilimia 46 na Antony Mallya asilimia 12.  Baada ya marudio Welwel aliibuka kidedea kwa asilimia 51

Mkutano huo wa uchaguzi, ulitanguliwa na wa viongozi wa mabaraza ya wanawake (Bawacha), vijana (Bavicha) na wazee (Bazecha).

Wengine waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Gervas Sulle (Makamu Mwenyekiti), na Emma Kimambo mwekahazina. Uchaguzi huo ulisimamiwa na mjumbe wa kamati kuu, Patrick Ole Sosopi.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Welwel amesema hatarajii kuwepo kwa makundi ndani ya chama hicho na amewataka viongozi kutokumwambia nani mzuri au nani mbaya.

“Niwaombe wajumbe na viongozi wa majimbo na mikoa, sasa uchaguzi umeisha, tuna jukumu moja la kuimarisha chama chetu, kusonga mbele, adui yetu ni mmoja—CCM na wadhalimu ambao wanahujumu haki za Watanzania, nisitarajie tukitoka hapa tuendelee na makundi yetu.

“Sitaki kurithi maadui, msiniambie nani mzuri nani mbaya, mimi mwenye nina akili ya kupima, wale wote walioko tayari tutafanya kazi kwa pamoja, msiniambie nani kanipigia kura nani hajanipigia kura, sitamani kusikia hilo, ninaamini kila nitakayekutana naye nitaweka imani kwamba amenichagua na ndiyo maana nimeshinda,” amesema.

Kuhusu migogoro, mwenyekiti huyo amesema anatambua kuna migogoro michache na kuwa watashirikiana kuweka mikakati kuhakikisha wanaondoa tofauti zilizopo baina ya viongozi wa mikoa na majimbo ili wawe kitu kimoja na kuijenga Kanda hiyo.

“Kuna watu wanaamini kwamba kiatu cha Lema kilikuwa kikubwa sana, yeye ni imara kwenye eneo lake na niwahakikishie mjivunie wana Kaskazini na mimi ni imara kwenye eneo langu, pengine nisiweze aliyoyafanya yeye lakini kuna mambo mimi naweza kuyafanya yeye asiweze kuyafanya,” amesema.

Kabla ya uchaguzi huo, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisoma ujumbe wa Lema ambaye hakuhudhuria uchaguzi huo kwa kuwa amekwenda kuiona familia yake Canada.

“Nilisafiri kuja kumuona mke wangu mpendwa na watoto na kupumzisha akili yangu kidogo, kwani niliona napaswa kufanya hivyo kwa sababu ya amani ya moyo wangu. Leo mtachagua viongozi wa Kanda yetu na ningekuwepo ningepiga kura na kama ninaweza kupiga kidijitali nitafurahi kufanya hivyo.

“Hata hivyo, ninakiri kuona na kusikia majina ya wagombea wote mliiomba nafasi katika uchaguzi huu sina maoni yoyote kwa uchaguzi huu, japokuwa najua nani ningempa kura kama ningekuwa hapo, na nani asingestahili kwa upande wangu.

Lema ameeleza kwenye ujumbe wake huo, kwamba amekuwa kwenye kazi ya harakati kwa zaidi ya miaka 20, hajawahi kuigiza kwenye mapambano kwani amezika na kuuguza rafiki zake wengi wakipigania haki na ustawi wa nchi hii.

Amesema anajali uadilifu wa kazi hii, lakini amepigwa, amekwenda polisi na mahabusu mara nyingi lakini hajawahi kujuta.

Lema amesema anafahamu yeye si malaika na anaweza kuwa amewaumiza au kuwakwaza watu wengi miongoni mwao, lakini anaweza kula kiapo cha familia yake kuwa hajawahi hata siku moja kuwaza hila kwa mmoja wao, zaidi ya kujali ubora na mkakati wa kuimarisha kazi hiyo muhimu.

“Viongozi mtakaochaguliwa leo, lindeni sana nidhamu ya kanda yetu, mwenyekiti mwingine na kiongozi yoyote wa ngazi yoyote asitukanwe wala kudhalilishwa, maana matusi na dhihaka vinaua sana morali ya kuwajibika, pengine ni udhaifu kukimbia changamoto ila ni hekima kuwaonyesha rafiki na maadui zako kuwa leadership is not a title (uongozi siyo cheo),” amesema.