Mtanzania achaguliwa Mkurugenzi Mkuu ECSA– HC

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya Tanzania, Dk Ntuli Kapologwe, ameibuka mshindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC), baada ya kuwashinda wagombea wengine sita.

Dk Ntuli anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Yoswa Dambisya wa Uganda, aliyemaliza mihula miwili ya miaka 10. Ataongoza kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa makubaliano ya Jumuiya hiyo.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, akizungumza leo Jumatano Februari 12, 2025 mara baada ya ushindi huo amesema nafasi hiyo ilivutia waombaji 47, lakini baada ya mchujo, saba walichaguliwa kuendelea. Hatimaye, Dk Ntuli aliingia hatua ya mwisho na wagombea wawili kutoka Kenya na Malawi, ambapo alipata kura nyingi zaidi.

Ushindi huu unaifanya Tanzania kuthibitisha uwepo wa wataalamu wake wenye sifa za kushika nafasi za uongozi wa kimataifa. Ni mara ya pili kwa Mtanzania kushika wadhifa huu, baada ya Dk Winny Mpanju (1983-2000).

Jumuiya ya ECSA – HC iliyoanzishwa mwaka 1974, inajumuisha nchi tisa wanachama, ikishirikiana na mataifa mengine 13.

Endelea kufuatilia Mwananchi.