DK. Nchimbi Akutana Nakuzungumza Na Mabalozi – Global Publishers



Mabalozi wa Uganda, Algeria, India, na Marekani wamepongeza uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, mabalozi hao walitoa pongezi pia kwa Dkt. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Tanzania, pamoja na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Balozi wa Algeria, Ahmed Djellal, alisisitiza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Algeria, huku akizungumzia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kubadilishana uzoefu wa kiuongozi.

Balozi wa India, Bishwadip Dey, alieleza kuwa uhusiano wa Tanzania na India unazidi kuimarika, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia, na afya.


Naibu Balozi wa Marekani, Andrew Lentz, alibainisha umuhimu wa kudumisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Marekani katika nyanja mbalimbali.

Balozi wa Uganda, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, alifikisha salamu za pongezi kutoka Serikali ya Uganda na chama tawala cha NRM, akitambua mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika.