Mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X siku ya Jumamosi Februari 15, 2025 kwamba ataushambulia mji wa Bunia, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, iwapo “vikosi vyote” vilivyopo huko havitakuwa vimejisalimisha ndani ya saa 24.
Kainerugaba, ambaye mara kwa mara ametoa matamshi yenye utata kuhusu sera za kigeni, alisema anafanya hivyo kwa mamlaka ya Rais Yoweri Museveni, ambaye pia ni baba yake. Msemaji wa jeshi la Uganda aesema hawezi kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Mapema Jumamosi, Kainerugaba alidai bila kutoa ushahidi kuwa watu wa kabila la Bahima wanauawa.
“Watu wangu, Bahima, wanashambuliwa. Hali hiyo ni hatari sana kwa wale wanaowashambulia watu wangu. Hakuna mtu duniani anayeweza kuwaua watu wangu na kufikiri hataathirika kwa hilo!” alisema.
Katika chapisho jingine, alisema, “Bunia hivi karibuni itakuwa mikononi mwa UPDF,” akirejelea Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda.
Tishio hili kutoka kwa afisa wa juu wa jeshi la Uganda, ambaye wengi wanaamini kuwa mrithi wa baba yake, limeongeza hofu kwamba mgogoro kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda unaweza kupanuka na kuwa vita vya kikanda.
Ijumaa Feb 14, kiongozi wa M23 alisema waasi hao wameingia Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa mashariki mwa Kongo, baada ya kuiteka Goma mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mapema Februari, shirika la habari la Reuters, likinukuu vyanzo vya Umoja wa Mataifa, liliripoti kuwa Uganda ilikuwa imepeleka zaidi ya wanajeshi 1,000 mashariki mwa Kongo chini ya operesheni ya kusaidia Kongo kupambana na wanamgambo wa Kiislamu.
Hata hivyo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema Uganda pia inaunga mkono M23, kundi linaloongozwa na Watutsi.
Kainerugaba ameonyesha wazi uungwaji mkono wake kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye amekanusha madai kwamba wanajeshi wa Rwanda wanapigana bega kwa bega na M23.