Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar na mkoa wa Pwani yanatarajiwa kukumbana na changamoto ya huduma ya umeme kwa siku sita mfululizo.
Kufanya maboresho katika kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Msongo wa Kilovoti 220 cha Ubungo kilichopo Jijini Dar es Salaam ni sababu ya kuathirika kwa kukosa umeme kwa nyakati tofauti kwa siku hizo.
Isitoshe katika kipindi hicho, katika kipindi hicho ambacho huduma ya umeme itakosekana kwa nyakati tofauti Shirika la Umeme Tanesco litakuwa likifanya matengenezo mbalimbali ya miundombinu ya umeme kwenye maeneo tajwa.
Katika maboresho hayo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), litafunga mashineumba (Transformer) mpya kubwa yenye uwezo wa MVA 300 ili kukidhi mahitaji ya umeme katika maeneo tajwa na kutibu tatizo la kuzidiwa kutokana na ongezeko la mahitaji.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma (Tanesco) Makao Makuu Dodoma leo, Jumatano Februari 19, 2025 imesema maboresho ya kituo hicho yataanza kuanzia siku ya Jumamosi, Februari 22 hadi 28 Mwaka huu.
“Hatua hii ni muhimu kwa Shirika katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake kufuatia ongezeko la mahitaji ya matumizi ya umeme katika maeneo ya Zanzibar na Mikoa ya Dar es Salaam, na Pwani ambalo limepelekea Kituo hicho kuzidiwa na hivyo kulazimu kufungwa kwa Mashineumba (Transformer) mpya kubwa yenye uwezo wa MVA 300 ili kukidhi mahitaji ya umeme katika maeneo tajwa.,” amesema.
Amesema katika taarifa hiyo imesema wakati kazi hizo zitakapofanyika baadhi ya maeneo ya Zanzibar na Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani yataathirika kwa kukosa umeme kwa nyakati tofauti.
“Katika kipindi hicho ambacho huduma ya umeme itakosekana kwa nyakati tofauti Shirika pia litakuwa likifanya matengenezo mbalimbali ya miundombinu ya umeme kwenye maeneo tajwa ili kuiweka miundombinu yetu kwenye hali ya uimara hasa kwenye kipindi hiki tunachoelekea cha msimu wa mvua.,” imesema.
Kufutia mabadiliko hayo shirika hilo linaomba radhi kwa usumbufu katika kipindi chote ambacho huduma ya umeme itakosekana kwenye baadhi ya maeneo na litaendelea kutoa taarifa za maendeleo ya kazi hiyo mpaka kukamilika kwake.