Kamati Kuu Chadema kukutana Dar, Dk Slaa atajwa

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inakutana katika kikao maalumu cha siku mbili kuanzia leo Jumatatu Machi 10-11, 2025 kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo usaili wa wagombea katika kanda ya Unguja.

Kanda hiyo ni sehemu ya kanda 10 za Chadema ambazo nyingine tisa zimeshamaliza uchaguzi wake na ilibaki ya Unguja pekee. Katika kikao hicho chini ya uenyekiti wa Tundu Lissu ndiyo itakaowasaili wagombea wote.

Taarifa za kikao hicho, imetolewa leo Jumatatu, Machi 10, 2025 na Msaidizi wa Kurugenzi ya Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, Apolinary Margwe, ikisema kikao hicho kitafanyikia makao makuu ya chama hicho Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia usaili wa wagombea wa kanda ya Unguja, Margwe amesema katika kanda 10 zilizopo ndani ya chama hicho, ni Unguja pekee haikumalizia kufanya uchaguzi kama ilivyokuwa kwa nyingine zilizomaliza mchakato huo mwaka jana.

“Walikuwa wamefanya uchaguzi ngazi ya chini na waliishia mikoa, lakini baada ya kamati kuu kukaa sasa itafanya usaili wa majina ya wagombea na wakishamaliza itapangwa siku ya uchaguzi wenyewe,” amesema.

Kanda nyingine za chama hicho ambazo zimeshafanya uchaguzi ni Serengeti, Victoria, Kaskazini, Kusini, Nyasa, Magharibi, Pwani, Pemba na kanda ya Kati.

Taarifa ambazo Mwananchi inazo ni kwamba, katika kikao hicho huenda suala la aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa la kurejea kundini likajadiliwa.

Dk Slaa ambaye katikati ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, alitangaza kujiweka kando akipingana na masuala kadhaa. Baadaye Novemba 23, 2017 aliteuliwa na Rais wa wakati huo, John Magufuli, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Hata hivyo, baada ya kumaliza muda wake wa utumishi wa ubalozi, alirejea Tanzania na Septemba mosi, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kumvua hadhi ya ubalozi.

Hoja ya suala la Dk Slaa kujadiliwa katika kikao hicho inajili kipindi ambacho kumekuwa na sauti zinazosadikika kuwa za Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa, na Makamu Mwenyekiti -Bara, John Heche wakisikika wakijadili suala hilo.

 Katika sehemu ya sauti hizo ambazo zimesambaa mitandaoni, anasikika Golugwa akimweleza Heche jinsi ya Dk Slaa aandike barua ya kuomba kurejea tena Chadema ili waipeleke kwenye sekretarieti na iwe sehemu ya ajenda kwenye kamati kuu.

Hata hivyo, Mwananchi limewatafuta Heche na Golugwa bila mafanikio. Alipoulizwa hilo, Margwe amesema mambo mengine yatakayojadiliwa kupitia kikao hicho yatatangazwa baadaye baada ya kumalizika mkutano huo.

Suala hilo la Dk Slaa kurejea Chadema liliwahi kuelezwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema, wakati wa kampeni za uchaguzi wa chama akisema endapo Lissu aliyekuwa akiwania uenyekiti kama atashinda atamshauri amteue kuwa mjumbe wa kamati kuu.

Uchaguzi mkuu wa Chadema uliofanyika Januari 21, 2025 na Lissu akiibuka mshindi dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21.

Baada ya ushindi wa Lissu, kundi ambalo lilikuwa likimuunga mkono limekuwa likimpigia chapuo kwamba anafaa kurejea kuendelea jitihada za kupigania demokrasia.

Dk Slaa mwenyewe, Februari 27, 2025, baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na kufutiwa kesi ya jinai na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), alisema yuko tayari kurejea Chadema.

DPP alimfutia kesi ya jinai namba 993/2025 yenye shtaka la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa X, baada ya kukaa gerezani kwa siku 48.

Nje ya mahakama, akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kuachiwa huru na Mahakama, Dk Slaa alisema yupo tayari kurudi Chadema. “Kile tulichokipigania wamekiweka wazi, sasa hivi kile kilichoniondoa mwaka 2015 kimeshafutika, sasa hivi sina tatizo lolote kufanya kazi karibu zaidi na Chadema kwa utaratibu wa Chadema,” alisema Dk Slaa.

Alipoulizwa iwapo atarudi Chadema, Dk Slaa alijibu: “Huko mwanzo nilikuwa kwenye uanaharakati, sasa nipo tayari kurudi Chadema.”

Machi 8, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) waliliadhimisha kitaifa jijini Dar es Salaam, Dk Slaa alikuwa sehemu ya wageni waalikwa.  Katika sherehe hizo, alipata wasaa wa kuzungumza na kusema yuko tayari kushirikiana na Chadema kwenye harakati zote ikiwemo ya “No reform no election.”

Moja ya hoja nyingine inayoweza kujitokeza kwenye kamati kuu hiyo ni kujazwa kwa wajumbe wa sekretarieti. Hii inatokana na wajumbe waliokuwapo baada ya kumalizika kwa uchaguzi kujiweka kando na wengine walijiuzulu.

Katika kurugenzi tano za Chadema, tayari imeshajazwa nafasi moja ya uchumi na fedha, huku kurugenzi nyingine zikiendelea kuwa wazi tangu Januari 21, 2025.

Wajumbe hao wanapatikana kwa Mwenyekiti Lissu kushauriana na Katibu Mkuu, John Mnyika, kuwasilisha majina wanayoona yanafaa ili kamati kuu iweze kuwateua.

Hivyo, kutokana na uenyeti wa kurugenzi hizo na harakati za chama hicho, kuna uwezekano suala hili nalo likajadiliwa na kujazwa. Kurugenzi hizo tano ni: fedha, uwekezaji na utawala, sheria na haki za binadamu, mawasiliano, itifaki na mambo ya nje, uchaguzi, na ile ya ufuatiliaji na tathmini.

Kampeni ya tone tone iliyozinduliwa hivi karibuni kwa ajili ya kukusanya fedha ili kusaidia kampeni ya “no reform no election” huenda likawa sehemu ya mjadala hususan jinsi ya kwenda kuanza utekelezaji wake kwa wananchi.

Lissu wakati anaizindua alisema fedha hizo zitawezesha kufanyika kwa mikutano ya hadhara nchi nzima, kuhamasisha wananchi kueleza “no reform no election” kwamba maana bila mabadiliko ya kimfumo hakuna uchaguzi.

Machi 3, 2025, Golugwa akitoa mrejesho wa tone tone alisema Sh64 milioni zilikuwa zimechangwa kwa siku saba tangu kuzinduliwa kwake, watakwenda kuanza mikutano ya hadhara mikoa ya Kusini.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.

Related Posts

▪️Serikali kupunguza ada ya kodi ya pango kwa mwaka kwa Leseni ya chumvi ▪️Rais Samia apongezwa kwa kiwanda cha kusafisha chumvi Lindi ▪️Wazalishaji wa chumvi wafurahia kuanza kwa kodi ya zuio ▪️Serikali kudhibiti uingizaji wa chumvi kiholela nchini Dar es Salaam Katika kuwajengea uwezo wazalishaji wa chimvi nchini,Serikali imekuja na mikakati mbalimbali kufikia azma hiyo ikiwemo upunguzaji wa ada ya pango kwa mwaka ya leseni (Annual Rent) za uchimbaji mdogo wa chumvi nchini ili kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji wa wingi wa chumvi nchini. Hayo yamesemwa jana tarehe 15 Julai, 2025 na Waziri wa Madini, *Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)* Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga Kikao cha wadau wa sekta ndogo ya chumvi chini ya Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA). "*Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan* ameendelea kutubeba sekta ya madini na wachimbaji kwa ujumla. Ni yeye aliyetuelekeza kusikilize kilio chenu na kutatua changamoto zinazowakabili ili mnufaike na shughuli mnazofanya" "Ametuelekeza Wizara ya Madini tuliridhie ombi lenu na kupunguza ada ya pango ya mwaka ya leseni ya uchimbaji mdogo kutoka Shilingi 45,000 mpaka Shilingi 20,000 kwa hekta, hili linakwenda kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ubora wa chumvi ya mzalishaji mdogo" alieleza Mhe. Mavunde. Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo udhibiti wa chumvi inayoingizwa kutoka nje ya nchi, zimepelekea bei ya chumvi ghafi kuongezeka na hivyo kuwanufaisha zaidi wazalishaji wadogo wa chumvi nchini. Uanzishwaji wa kodi ya zuio ya asilimia mbili (2%) kwenye mauzo ya chumvi ghafi kwa wazalishaji wenye leseni za PML imekuwa ni neema na manufaa kwao badala ya utaratibu wa awali wa kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato, ambao ulikuwa ni kero kubwa kwa wazalishaji wadogo. Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde alieleza kuwa Kiwanda cha kuzalisha chumvi cha STAMICO kipo hatua za mwisho, na kuagiza Shirika hilo kuhakikisha kabla ya mwezi wa Agosti kuisha kiwe kimekamilika na kuanza uzalishaji wa chumvi ili kupanua wigo wa soko la chumvi ya wazalishaji wadogo. Awali, akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi yao, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA), Bi. Hawa Ghasia aliishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta ndogo ya chumvi nchini ambazo zimepelekea bei ya chumvi kupanda na kuwanufaisha zaidi wazalisha chumvi nchini.