Ajira 41,500 kada mbalimbali mbioni kutangazwa

Dodoma. Katika Mwaka wa Fedha 2025/26 Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imepanga kushughulikia vibali 41,500 vya ajira ili kujaza nafasi zilizoidhinishwa katika Ikama.

Mbali na ajira hizo mpya, Serikali imepanga kuhakiki na kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi kwa taasisi 425 na kusafisha taarifa za kiutumishi na mishahara (Data Cleaning) kwa watumishi waliopo katika taasisi 433 zinazotumia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-Watumishi).

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatano Aprili 23, 2025 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene wakati akiwasilisha maombi ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 na kuomba Bunge liidhinishe Sh1.354 trilioni kwa mafungu yote.

Kati ya fedha hizo Sh1.17 trilioni matumizi ya kawaida na Sh183.3 bilioni ni fedha za miradi ya maendeleo.

Katika taarifa yake, Simbachawene amekiri bado kuna upungufu wa watumishi kwa baadhi ya kada, hivyo bajeti inayopitishwa inakwenda kupunguza pengo hilo pamoja na kuhakiki na kuidhinisha mabadiliko ya taarifa zinazohusu utumishi na mishahara katika Mfumo wa e-Watumishi kwa taasisi 524.

Hata hivyo, wabunge wamekosoa mfumo unaotumika katika kuajiri watumishi wapya wakisema si rafiki na kwamba sekretarieti ya ajira ni kama wamesahau jukumu lao na kulikabidhi kwa watu wengine.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka ombwe kwenye nafasi zinazotangazwa kwa ajili ya ajira mpya zinazotajwa zinatolewa kwa kujuana huku watoto wa masikini wakikosa nafasi.

Malalamiko hayo yaliibukia bungeni baada ya Mbunge wa Msalala Kasalali Mageni kuibua tuhuma za ajira kutolewa kwa upendeleo na kujuana huku akieleza simu za wabunge kwamba zimejaa jumbe (sms) za wasaka ajira.

“Pamoja na hayo, tutafanya uhakiki maalumu wa watumishi katika taasisi za umma za Mkoa wa Dodoma lakini tutawezesha taasisi 35 ambazo kwa sasa hazitumii Mfumo wa e-Watumishi kuanza kutumia mfumo tajwa katika kusimamia masuala ya kiutumishi na mishahara,” amesema Simbachawene.

Waziri amesema Serikali itaendelea kutoa ajira kwa namna itakavyowezekana kulingana na mahitaji na upatikanaji wa bajeti lakini kuendelea kurekebisha mifumo kulingana na mahitaji.

Waziri amesema bajeti hiyo inakwenda kufanya uchambuzi wa miundo ya wizara na taasisi za umma 30 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ikiwamo kutoa mafunzo ya mbinu za uongozi na utawala bora kwa viongozi wa Serikali watakaoteuliwa baada ya uchaguzi.

Kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Waziri amesema chombo hicho kimepiga hatua kubwa katika majukumu yake kwa kuwa, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, walifuatilia miradi 1,407 yenye thamani ya Sh2.007 trilioni.

Amesema katika ufuatiliaji huo, miradi 129 yenye thamani ya Sh44.76 bilioni ilibainika kuwa na kasoro.

Kwa kipindi hicho pia Takukuru ilifanikiwa kushinda kesi 352 kati ya 451 zilizoendeshwa mahakamani wakati kesi 10 zilibainika kuwa ni kubwa, hivyo kupelekwa divisheni ya makosa ya uhujumu uchumi.

Utekelezaji wa bajeti hiyo ni pamoja na kutoa mafunzo ya kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma kwa viongozi 364 wa Serikali lakini itasaidia kwa upande wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ambako kutatolewa ruzuku kwa kaya maskini 906,669 zinazokidhi vigezo vya Mpango.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Florent Kyombo amesema Serikali itengeneze mfumo wa malipo ambao utakuwa ni mwongozo kwa ofisi za umma na Serikali kwa lengo la kuwasaidia vijana wanaojitolea katika nafasi mbalimbali.

Kyombo ambaye amesoma taarifa ya kamati, ameitaka Serikali kutengeneza mfumo wa ajira za watumishi wa kada mbalimbali katika utumishi wa umma usimamiwe na taasisi moja ili kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.

“Kwa kuwa vijana wengi wamekosa ajira, Serikali iangalie namna nzuri ya kuwafanyia mafunzo na kuwatafutia nafasi katika soko la ajira nje ya nchi, ili kuwakwamua vijana kutoka katika wimbi la kukosa ajira,” amesema Kyombo.

Kamati imeitaka Serikali kuendelea kuimarisha misingi ya utawala bora pamoja na kuboresha mifumo ya utendaji kazi katika utumishi wa umma sambamba na kuboresha mishahara na masilahi ya watumishi.