TUME YAANZA KUKUTANA NA WADAU KATIKA MAJIMBO YALIOOMBA KUGAWANYWA



0

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akiongoza kikao cha pamoja kati ya Tume na wadau wa uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza ambacho kililenga kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ya kuligawa jimbo la Magu ni sahihi kuhusu jimbo husika. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Ndg. Joshua Nassari na katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndg. Greyson Ocardo.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndg. Greyson Ocardo (kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Ndg. Joshua Nassari

Mbunge wa jimbo la Magu
Mhe. Boniventura Destery Kiswaga akizungumza wakati wa mkutano huo ambapo aliunga mkono hoja ya ugawaji wa jimbo hilo kama ilivyowasilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa kwa Tume. 

Baadhi ya washiriki ambao ni wadau wa Uchaguzi wakichangia mada wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wadau wa uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza ambapo Tume ilikutana nao ili kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ya kuligawa jimbo la Magu ni sahihi kuhusu jimbo husika. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana.

Baadhi
ya washiriki ambao ni wadau wa Uchaguzi wakichangia mada wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na
Wadau wa uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza ambapo
Tume ilikutana nao ili kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi
yaliyowasilishwa ya kuligawa jimbo la Magu ni sahihi kuhusu jimbo husika. Kulia
ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana.

Na Mwandishi wetu, Magu
Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Aprili 23,2025
ameongoza kikao cha pamoja kati ya Tume na Wadau wa Uchaguzi katika Halmashauri
ya Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa
zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ya kuligawa jimbo la Magu ni sahihi
kuhusu jimbo husika.

 

”Tulipokea maombi ya
mapendekezo ya kugawa jimbo la uchaguzi la Magu kupitia barua yenye Kumb. Na.
CFA.89/231/01C/20 ya tarehe 11 Machi, 2025 kutoka kwa Katibu tawala Mkoa wa
Mwanza, hivyo kikao hiki ni kifupi, lengo lake ni kujiridhisha na takwimu na
jina la jimbo kama mlivyowasilisha ikiwa ni sehemu ya jukumu la Tume la
kuwashirikisha wadau wake wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.

 

Alisema, Tume imechagua kutembelea
baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa
zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ni sahihi kuhusu jimbo husika.

 

Jaji Mwambegele alisema kwa
mujibu wa ibara ya 75(4) na 74(6)(c) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024, Tume ina jukumu la
kuchunguza na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi. Aidha,
Tume inaweza kutekeleza jukumu hilo mara kwa mara au angalau kila baada ya
miaka kumi.

 

”Aida, ibara ya 75(3) na (4)
imeainisha vigezo vya ugawaji wa majimbo ambavyo ni idadi ya watu, upatikanaji
wa mawasiliano, na hali ya kijiografia. Vigezo vingine vinavyozingatiwa na Tume
katika kugawa majimbo vimeainishwa katika Jedwali la Tatu la Kanuni za Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024,”alisema Jaji Mwambegele.

 

Jaji Mwambegele alivitaja
vigezo vingine vinavyohusika katika ugawaji wa majimbo kuwa ni pamoja na hali
ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja
kutokuwa ndani ya Wilaya au Halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya
watu yaliyopo, mazingira ya muungano, uwezo wa ukumbi wa Bunge; na  idadi ya viti maalum vya wanawake.

 

Miongoni mwa waliohudhuria
kikao hicho ni pamoja na viongozi wa Mkoa wa Mwanza, Viongozi wa Wilaya ya
Magu, Viongozi wa Vyama vya Siasa Magu, Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya
wanawake, vijana, wenye ulemavu na wazee wa Kimila.

 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC) ilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili
majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipokea 
mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.

Related Posts