Dar es Salaam. Serikali imewakumbusha waajiri nchini kujiweka tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia huku wakichukua tahadhari dhidi ya athari zake hasi zinazoweza kutokea ikiwemo upotevu wa baadhi ya fursa za ajira.
Wito huo umetolewa Aprili 28, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete wakati akiwaongoza mamia ya Watanzania kwenye maadhimisho ya siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani, iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Singida katika viwanja vya Mandewa.
Akihutubia katika kilele cha maadhimisho hayo, Ridhiwani amesema Serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi yake, hivyo imeendelea kuuwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan, anatambua na kujali afya na usalama wa wafanyakazi nchini na amethibitisha hilo kwa vitendo kupitia uwezeshaji ambao amekuwa akiufanya kwa OSHA, ikiwamo kuipatia vitendea kazi na kuwaongezea watumishi ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia Watanzania,” amesema.
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu isemayo: “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi”, Ridhiwani amesema teknolojia ina mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa utendaji.
“Ninawashauri waajiri nchini kujiweka tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia huku wakichukua tahadhari dhidi ya athari hasi za teknolojia ikiwemo kupotea kwa baadhi ya fursa za ajira,” amesema Ridhiwani.
Waziri huyo amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kuandaa sera zinazowajumuisha wajasiriamali wadogo katika fursa mbalimbali za kiuchumi yakiwemo masuala ya usalama na afya kazini.
Hatua hiyo inatekelezwa na OSHA ambayo imeanzisha programu maalumu ijulikanayo ‘Afya Yangu, Mtaji Wangu’ ili kuyatambua makundi ya wajasiriamali wadogo na kuyawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.
Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi nchini.
Ameanisha shughuli ambazo ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka huu kuwa ni pamoja na maonyesho ya usalama na afya mahali pa kazi, kliniki ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, shindano la tuzo za usalama na afya mahali pa kazi, bonanza la michezo pamoja na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Kanda ya Afrika Masharika, Caroline Khamati Mgalla ameipongeza Serikali ya Tanzania na wadau wa usalama na afya nchini, kwa maandalizi mazuri ambayo yamehusisha shughuli zenye tija kwa jamii zikiwemo huduma ya upimaji afya na matibabu kwa wananchi na mafunzo kwa wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba amewapongeza waajiri kwa mwitikio mzuri katika maadhimisho ya mwaka huu huku akiwashauri kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo akili unde ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya ametoa tahadhari kwa waajiri nchini kuhakikisha teknolojia mpya zinazotumika katika uzalishaji haziathiri ajira za Watanzania.
Aprili 28, 2025 kila mwaka hutambulika kimataifa kama Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo.
Lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi, pamoja na kuwakumbuka walioumia au kupoteza maisha wakiwa wanatekeleza majukumu yao.