Dar es Salaam. Changamoto za kifedha, kuingiliwa kisiasa, shinikizo katika baadhi ya taasisi, uoga na kutokuwa na utulivu wa kisiasa zimetajwa kuwa vikwazo vya uhuru wa kitaaluma katika nchi mbalimbali za Afrika.
Kwa mujibu wa wanazuoni wa kada mbalimbali, ingawa imepita miongo mitatu tangu kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam na Kampala kuhusu uhuru wa wanataaluma na wajibu wao katika jamii, bado kuna vikwazo vinavyoukabili.
Kwa sababu ya vikwazo hivyo, wasomi hao wamesema ndiyo sababu ya kuwepo kwa ombwe la sauti za wanazuoni katika mataifa ya Afrika, hasa yanapotokea mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Hoja hizo za wanazuoni zinakuja katika kipindi ambacho kumeibuka mitazamo ya wadau mbalimbali wanaodai wasomi wengi kwa sasa wanakosa uhuru kwa sababu wamejitega kusubiri teuzi mbalimbali.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam na baadhi ya wanazuoni na wasomi waliohudhuria mkutano wa siku nne wa kujadili Uhuru wa Kitaaluma katika Bara la Afrika unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika mchango wake kwenye mkutano huo, Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii UDSM, Profesa Christine Noe amesema kwa muda sasa kumekuwa na ombwe la sauti za wanataaluma katika nchi mbalimbali za Afrika licha ya kutokea matukio makubwa ya kijamii, uchumi na siasa.
Amesema baadhi ya wanataaluma hawazungumzi kwa sauti zinazosikika kuhusu masuala hayo kama wanavyopaswa kufanya kwa mujibu wa nafasi zao katika jamii.
“Kazi yetu kama wanataaluma inalega, sauti zetu hazisikiki, mawazo yetu hayaendi mbali. Hiyo ndiyo sababu tumeitana kwa pamoja kujadili,” amesema.
Katika baadhi ya nchi, Profesa Christine amesema kumekuwa na muingiliano wa taaluma, Serikali na uendeshaji wa vyuo vikuu unaopoteza uhuru wa vyuo husika kujiendesha.
“Vyuo vikuu asili yake ni kujitegemea katika kutengeneza taaluma na kufanya tafiti bila kuingiliwa,” ameeleza.
Kukosekana kwa uhuru wa wanataaluma, kwa mtazamo wa Mtaalamu wa Elimu Dk Thomas Jabir, kunasababishwa na changamoto ya utulivu wa kisiasa inayoyakumba mataifa kadhaa ya Afrika.
“Mipaka ya demokrasia katika nchi nyingi za Afrika ikichangiwa na vurugu za uchaguzi, mapinduzi ya kikatiba yanayoongeza mamlaka ya viongozi wakuu, na ufuatiliaji wa wasomi ni vikwazo vikubwa,” amesema.
Licha ya wanazuoni hao kuwa na mitazamo hiyo, mwanazuoni mkongwe aliyebobea katika taaluma ya sheria, Profesa Issa Shivji, ameshusha mzigo wa lawama kwa wanataaluma wenyewe, akisema wanakosa uhuru kwa uoga wao wenyewe.
Katika msisitizo wa hoja yake hiyo, mwanazuoni huyo amewataka wanataaluma kutambua wajibu wao na kuendeleza mijadala yenye tija kwa nchi bila kuhofia chochote, kwa kuwa kujadili ndiyo chanzo cha maendeleo ya taifa.
Wakati wanazuoni wakionyesha vikwazo hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Serikali ya Tanzania inaunga mkono uhuru wa kitaaluma huku akiahidi kurekebisha sheria, sera au mazingira yoyote ya kimfumo yanayowazuia wasomi kuwa huru kutoa maoni yao katika masuala mbalimbali.
Dk Tulia, akifungua kongamano hilo, amesema Tanzania inathamini mchango wa wanataaluma na wanazuoni katika maendeleo ya jamii na iko tayari kulinda uhuru wao wa mawazo.
“Bunge limejipanga kusaidia UDSM na vyuo vikuu vingine nchini endapo kutakuwa na uhitaji wa mabadiliko ya sera kwa lengo la kuboresha uhuru wao wa mawazo ya kisayansi katika kuchangia uimara wa jamii.
“Ikiwa mnahitaji mabadiliko yoyote ya sheria inayokwamisha mawazo yenu au mawasilisho ya mawazo yenu au utafiti wenu, basi tutakuwa tayari kusaidia,” ameahidi.
Kwa mujibu wa Dk Tulia, uhuru wa kitaaluma umejumuishwa katika sheria na sera za Tanzania kupitia mifumo ya sayansi na elimu, na kwamba kuna haja ya kuimarisha mifumo hiyo ili kuwalinda zaidi wasomi.
“Hili litawezekana kwa kupitia upya sheria, sera na vikwazo vya kimfumo vinavyodhoofisha uhuru wa wasomi kushiriki kwenye hoja za kitaifa,” amesema.
Pia amepongeza lengo la mkutano la kupitia upya Azimio la Kampala kuhusu Uhuru wa Kitaaluma na Uwajibikaji wa Kijamii lililopitishwa mwaka 1990 na kulihuisha kulingana na mazingira ya sasa.
“Bila uhuru wa kitaaluma, hakuna utawala wa kidemokrasia wala maendeleo endelevu,” amesema.
Spika huyo amesisitiza kuwa Azimio la Kampala halikuwa tu nyaraka ya kihistoria, bali ni wito wa kuchukua hatua kwa wasomi wa Afrika.
“Lilikuwa ni tamko, dai la wazi na lisilo na hofu kuwa wasomi wa Afrika lazima wawe huru kufikiri, kuuliza na kusema, lakini wafanye hivyo kwa kuzingatia wajibu wao kwa jamii,” amesema.
Amevihimiza vyuo vikuu vya Afrika kurejesha wajibu wao wa kijamii na kupinga mwelekeo wa kugeuka taasisi za kibiashara.
“Vyuo vikuu visihudumie tu masoko ya kitaaluma. Vinapaswa kuhudumia jamii,” amesema.

Awali, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema ili kuondokana na changamoto hizo kunahitajika mshikamano wa pamoja wa wanataaluma kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika.
Kuwepo kwa mikutano kama hiyo, amesema ni fursa kwa wasomi kutafakari walipofika, kukabiliana na changamoto zilizopo, na kuhuisha dhamira yao kwa misingi ya uhuru wa kitaaluma.