Dar es Salaam. Serikali imelaani tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, na kuagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linawatafuta waliohusika na tukio hilo, wakamatwe na kuhojiwa.
Akizungumza jana, Mei 2, 2025, wakati wa hafla ya kuwaaga watumishi wa umma waliostaafu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amelitaka Jeshi la Polisi kumtafuta mtu aliyeandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba “siku za Kitima zinahesabika”, pamoja na wote waliopanga au kutekeleza shambulio hilo.
“Mtu huyu atafutwe haraka, ahojiwe ametumwa na nani, na hatua kali za kisheria zichukuliwe,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa viongozi wa dini katika kulinda amani, maadili na mshikamano wa kitaifa, na kwamba vitendo vya chuki na uchochezi havitavumiliwa.
“Kumekuwepo na ‘Waraka feki’ uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukidaiwa ni waraka wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Maaskofu Tanzania kupitia taarifa yake kwa umma imekanusha kuwa waraka huo haukutolewa na TEC, na kuwataka wananchi, waumini na watu wote wenye mapenzi mema kupuuza kabisa waraka huo” amesema Bashungwa
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Padri Kitima alishambuliwa eneo la Kurasini, Temeke, jijini Dar es Salaam, zilipo ofisi za TEC makao makuu.
Mpaka sasa, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Rauli Mahabi kwa tuhuma za kumjeruhi Padri Kitima.

Katika hatua nyingine, Bashungwa amewaelekeza watendaji wote wa Wizara na vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wao kwa weledi, kwa kuzingatia sheria, ili kulinda amani na usalama wa nchi.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na kuchukua hatua zinazositahili dhidi ya wahalifu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi yetu” amesisitiza Bashungwa.
Vilevile, Bashungwa amekemea vikali vitendo vyote vinavyochafua taswira ya taifa, vikiwemo vya kudhuru watu au kusambaza taarifa zenye kuchochea uhasama wa madhehebu ya kidini.
“Ni wakati muafaka sasa, Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya kusimamia sheria zinazohusu mitandao ya kijamii ili kuhakikisha watu wote wanatii sheria bila shuruti na hivyo kuendelea kuwa na jamii yenye ustaarabu na kuheshimu utu wa kila mtanzania na hata mgeni” amesisitiza.