KIUNGO wa KenGold, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ amefunguka kuhusu kuumizwa kwa kitendo cha timu hiyo kushuka daraja, licha ya kubakiwa na michezo mitatu kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa 2024/25.
Kengold iliyopanda daraja msimu huu na kushuka kwa kuvuna pointi 16 tu katika mechi 27, baada ya kupoteza mechi nne mfululizo zilizopita mbele ya Azam (2-0), Dodoma Jiji (3-0), Tanzania Prisons (3-1), na Coastal Union (2-1).
Hii ni mara ya kwanza kwa timu anayoichezea Cabaye kushuka daraja, jambo linaloonekana kumgusa kiungo huyo mkabaji na kabla ya kujiunga nayo alitokea Azam na KMC, lakini sasa anashuhudia kipindi kigumu zaidi cha maisha yake ya soka.
“Licha ya kwamba tumekutana na changamoto nyingi msimu huu, kuwa sehemu ya timu inayoshuka daraja ni jambo la maumivu makubwa kwangu na kwa wachezaji wenzangu. Tumepambana, lakini hatujafanikiwa,” alisema Cabaye.