Vatican. Mchakato wa kumchagua Papa mpya wa Kanisa Katoliki umeanza rasmi lakini bila mafanikio, baada ya moshi mweusi kufuka kutoka bomba la moshi la Kanisa la Sistine usiku huu kuamkia Alhamisi, Mei 8, 2025.
Tukio hilo linaashiria kuwa awamu ya kwanza ya upigaji kura iliyofanyika Jumatano jioni haikufanikisha kumpata papa atakayerithi nafasi iliyoachwa na Papa Francis.
Makardinali 133 waliokusanyika kutoka nchi 70 duniani waliendesha mchakato huo wa siri, wakitafuta kupata mshindi kwa theluthi mbili ya kura asilimia 66.7 sawa na kura 89.

Muonekano wa moshi mweusi ukiwa unafuka kutoka kwenye bomba nje ya Kanisa la Sistine
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki kwa mkutano wa uchaguzi wa papa kuwa na uwakilishi mpana zaidi kijiografia. Wengi wa makardinali hao, walioteuliwa na Papa Francis, wanatoka maeneo yaliyokuwa hayajawahi kuwa na kardinali kama Mongolia, Tonga na Uswidi.
Hali ya nje na ndani ya Sistine
Nje ya Kanisa la Sistine, Uwanja wa Mtakatifu Petro ulijaa umati wa waumini waliokusanyika kushuhudia tukio hilo la kihistoria kupitia skrini kubwa, huku wakishangilia kila hatua ya mchakato, zikiwamo milango kufungwa na moshi kuanza kufuka.
Ndani ya Sistine, hali ilikuwa ya utulivu na uzito wa kiimani, makardinali wakiwa wamevalia mavazi mekundu, wakiimba nyimbo za Kilatini na kutoa kiapo cha usiri mbele ya picha ya Michelangelo ya “Hukumu ya Mwisho”.

Makardinali wakiwa ndani ya Kanisa la Sistine katika mchakato wa kumchagua Papa mpya wa Kanisa Katoliki.
Askofu Mkuu Diego Ravelli, msimamizi wa ibada za kipapa, aliamuru “extra omnes” – yaani, watu wote wasiostahili wakae nje kabla ya lango kufungwa na mchakato kuanza rasmi.
“Natumaini makardinali watachagua mtu ambaye ni mpatanishi na ataunganisha Kanisa tena,” alisema Gabriel Capry (27), kijana kutoka London aliyekuwepo kwenye uwanja huo.
Mtalii Lisette Herrera kutoka Jamhuri ya Dominika alisema: “Ninamsihi Roho Mtakatifu atupe papa kijana atakayekaa nasi kwa muda mrefu.”
Ingawa makardinali wanapaswa kuepuka ushawishi wa kidunia, mikakati mbalimbali ya kushawishi ilionekana Roma kabla ya mkutano. Vijana Wakatoliki waliandika barua ya wazi, vyombo vya habari vya kihafidhina vikatoa tathmini za wagombea, na watetezi wa upadrisho wa wanawake walirusha moshi wa rangi ya waridi kutuma ujumbe wao.

Muonekano wa moshi mweusi ukiwa unafuka kutoka kwenye bomba nje ya Kanisa la Sistine
Rais wa Marekani, Donald Trump, naye alivutia hisia alipopigwa picha akiwa amevaa kama Papa kitendo kilicholaaniwa na wanasiasa wakongwe wa Ulaya kama kuingilia imani isivyofaa.
Kwa upande wa changamoto, Papa mpya anatarajiwa kukabiliana na masuala nyeti kama nafasi ya wanawake katika Kanisa, haki za watu wa LGBTQ+, wakimbizi, na kashfa ya unyanyasaji wa kingono. Swali kubwa kwa makardinali ni kama wataendeleza urithi wa mageuzi wa Francis au kuirejesha hali ya kihafidhina ili kuleta umoja katika Kanisa.
Wagombea wanaopewa nafasi kubwa ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin (Italia), ambaye ni Katibu wa Vatican, Kardinali Luis Tagle (Ufilipino), anayesifiwa kwa uongozi wake wa kiuinjilishaji barani Asia, na Kardinali Peter Erdo (Hungary), anayewakilisha msimamo wa kihafidhina.
Kwa mujibu wa historia, uchaguzi wa papa huwa unachukua kati ya awamu tatu hadi 14 za kupiga kura. Papa Francis mwenyewe alichaguliwa katika awamu ya tano mwaka 2013.
Makardinali wanatarajiwa kurejea Sistine Alhamisi asubuhi kuendelea na upigaji kura hadi pale watakapompata papa wa 267 wa Kanisa Katoliki duniani.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.