RASMI Simba SC ina tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao 2025-2026, hiyo ni baada ya kufikisha pointi 66 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ambazo haziwezi kufikiwa na timu zilizopo chini yake.
Simba imefikisha pointi hizo baada ya kuifunga Pamba Jiji mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika leo Alhamisi Mei 8, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Jean Charles Ahoua kwa kiasi kikubwa ndiye aliyeimaliza kazi hiyo baada ya kufunga mabao matatu dakika ya 16, 37 na 52 ambapo mawili yalitokana na mipira ya kutenga.
Bao la kwanza Ahoua alifunga kwa penalti baada ya Joshua Mutale kufanyiwa faulo eneo la hatari na winga Zabona Mayombya.