Mbeya City imehitimisha msimu kibabe baada ya kuikanda mabao 5-0 Green Warriors, huku viongozi wa timu hiyo na Chama Cha Soka mkoani humo wakieleza furaha na matarajio yao ya msimu ujao.
Timu hiyo ilishuka daraja misimu miwili nyuma ambapo msimu ujao itacheza tena Ligi Kuu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwa pointi 68 ikiachwa tatu na vinara Mtibwa Sugar.
Hata hivyo, kabla ya mechi ya leo kuhitimisha Ligi ya Championship, wachezaji, viongozi na mashabiki waliungana kufanya matebezi ya heshima mitaa mbalimbali ya Jiji la Mbeya kwa lengo la kushukuru wadau kwa sapoti.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, mabao Eliud Ambokile, Rifat Hamis, Malaki Joseph, Willy Thobias na Bruno Shayo.