Mtwara. Wataalamu kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari Naliendele) mkoani Mtwara wametakiwa kusimamia mazao mengine kama mpunga, karanga, mahindi, na mazao ya mbogamboga ili kusaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judithi Nguli ametoa wito huo leo Mei 13, 2025, wakati akifunga mafunzo ya maadili kwa wafanyakazi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele.
Nguli amesema kuwa baada ya msimu wa mazao ya ufuta na korosho, Mkoa wa Mtwara unapaswa kuwa na mikakati ya kulima mazao mengine ili kuongeza tija katika uchumi.

Baadhi ya wataalamu na watafiti wa kilimo kutoka Tari Naliendele waki wanafatilia mafunzo ya maadili kwa uma.
Amehimiza wataalamu wa kilimo kuhakikisha kuwa mazao ya chakula kama mpunga, mahindi, na mbogamboga yanapewa kipaumbele kwa kuwa yatasaidia kuongeza mapato na kuepusha matumizi ya fedha kununua chakula kutoka mikoa mingine.
Pia, Nguli amesisitiza umuhimu wa kuwa na maadili katika utumishi wa umma.
Amesisitiza kuwa hata kama mtu ana elimu ya juu, bila maadili, hakuwezi kufika mbali katika utumishi wa umma.
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele, Geradina Mzena amesema kuwa kutokana na mafanikio ya mazao kama korosho, mbaazi na ufuta, kituo kimeanzisha programu ya utafiti wa mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga ili kuwanufaisha wakulima wa Mtwara na Lindi.
Kwa upande wake, Rahimu Menya, ofisa mfawidhi kutoka Kituo Kidogo cha Nachingwea amesema mafunzo ya maadili yamewafundisha umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili mema na kwamba watafanikisha mabadiliko kwa wakulima.
Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti wa Kilimo Tari, Dk Thomasi Bwana amesema kuwa kwa sasa wanatekeleza majukumu yake kwa kufanya tafiti na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kilimo na kwamba wataalamu wanahitaji kuongeza ufanisi katika rasilimali watu, fedha na ardhi ili kufanikisha malengo hayo.