Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ameibuka kwa hoja baada ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kutoa shutuma kali dhidi ya utendaji wa wizara hiyo wakati wa kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza kwa ufasaha na utulivu wa kisomi, Dkt. Jafo amesema kuwa tabia ya kukosoa kila jambo la serikali bila kutambua juhudi na mafanikio ya wazi ni ishara ya kuwa na matatizo binafsi, na ni kukosa ubinadamu wa kisiasa.
Waziri huyo alieleza kuwa hoja zinazojengwa kwa msingi wa upinzani usio na uhalisia, huathiri taswira ya maendeleo na haziwasaidii wananchi wanaotegemea majibu na suluhisho, si lawama zisizo na tija.
Akiainisha mafanikio ya wizara yake, Dkt. Jafo alisema tayari serikali imetekeleza miradi mikubwa ya viwanda na kuimarisha sekta ya biashara kupitia sera na miongozo mipya, huku akisisitiza kuwa lengo la wizara ni kuchochea uchumi wa viwanda kwa vitendo, si maneno.
Kauli hiyo imeungwa mkono na baadhi ya wabunge waliochangia, wakieleza kuwa kuna haja ya kuacha siasa za kubeza kila jambo na badala yake kujenga hoja zenye mashiko kwa manufaa ya taifa.