Tume ya Rais ya kukusanya maboresho ya Kodi ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Maimuna Tarishi leo tarehe 16.05.2025 imekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ukiongozwa na Naibu Kamishna Mkuu Bw. Mcha Hassan Mcha Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kikao cha pamoja cha kukusanya maoni juu ya maboresho ya Kodi Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Maimuna Tarishi amesema ni mara ya pili kukutana na TRA kwa lengo la kujadili pamoja baadhi ya maoni waliyoyapata kwa wananchi na hii ni kutokana na kuwepo kwa uhusiano mkubwa baina ya TRA na Tume ya Rais.
Balozi Maimuna ameipongeza TRA kwa kazi kubwa ya kukusanya Kodi wanayoifanya na kueleza kuwa kupitia maoni wanayokusanya anaamini kazi hiyo itakapokamilika na kumkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutakuwa na maboresho makubwa.
