Dar es Salaam. Padri Anthony Mamsery, aliyeoongoza misa kumuombea muasisi wa kituo cha sala na maombezi cha Mama Bikira Maria (Marian Faith Healing), Padri Felician Nkwera (89), ameeleza sababu za mtumishi huyo wa Mungu kuzikwa na Kanisa Katoliki.
Padri Nkwera alifariki dunia Mei 8, 2025 katika hospitali ya TMJ alikokuwa akipatiwa matibabu. Maziko yake yamefanyika leo Jumamosi Mei 17, kituoni hapo, Ubungo Riverside, Dar es Salaam.
Padri Nkwera aliwahi kuhudumu katika Kanisa Katoliki kabla ya kutengwa na uongozi wa kanisa hilo.
Padri Mamsery, Mkuu wa Shirika la Msalaba Mtakatifu Puma, mkoani Singida amesema pamoja na changamoto alizopata ikiwamo kutengwa na kanisa wamemzika kwa heshima kwa kuwa mwili wa Mkristo unapaswa kuheshimiwa.
“Kuna watu siku hizi wamekuwa wakizika miili kwa kuitupa, kuichoma, lakini eleweni mwili wa Mkristo una thamani sana na unapaswa kuzikwa kwa heshima zote, ndivyo tulivyomfanyia mpendwa wetu hapa,” amesema.
Akimzungumzia Padri Nkwera amesema alipambana dhidi ya uovu, uasi, ushirikina, upagani na nguvu za giza zinazotesa watoto wa Mungu.
Amesema alisaidia watu wamjue Mungu na kumpenda, katika umri wake wa uzee ameeleza aliendelea kutii mamlaka za kanisa hivyo amekuwa mfano wa kuigwa.
“Magonjwa hupunguza utendaji wa watu na kusababisha ufukara kwa mgonjwa na familia inayomhudumia, lakini yeye alipambana na maradhi na magonjwa sugu ambayo yalishindikana hospitali,” amesema.
Amesema wagonjwa walipopelekwa kwake, aliposali na kuwapaka mafuta magonjwa yalitoweka na kwamba hiyo si kwa nguvu zake bali ni mkono wa Mungu.
Ameeleza Padri Nkwera hakujitangaza na alitumia karama aliyopewa bila kujificha, hata alipofikia uzee alihakikisha anampendeza Mungu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapunduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi aliyeshiriki misa amesema alimfahamu Padri Nkwera kwa mara ya kwanza mwaka 1983, akieleza ukiacha upadri alikuwa rafiki wa baba yake Mzee Nchimbi.
Amesema siku moja Padri Nkwera akiwa Kigoma kwa shughuli za maombezi alisafiri kwa treni, baba yake kwa urafiki waliokuwa nao alimsindikiza.
“Kabla hajaanza safari akakumbuka kati ya watoto wake mmoja anaumwa kichwa ambaye ni mimi, akaniambia twende ukabarikiwe. Nakumbuka padri alinipaka mafuta akasema kuanzia siku hiyo mimi ni mtoto wake,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Emmanuel Nchimbi (katika) na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakiwa katika Kituo cha Maombezi na Sala cha Bikira Maria kwa ajili ya misa ya kumuaga Padri Felician Nkwera.
Dk Nchimbi, ambaye pia ni mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, amesema hata kanisa linajua ni mtoto kwani katika shughuli zake alipomuona yupo kimya, aliwaambia wasaidizi wake wampigie simu na walizungumza mambo mbalimbali, ikiwamo kumuombea.
Amesema mara ya mwisho aliwasiliana na Padri Nkwera mwanzoni mwa Aprili akamwambia lazima afanyiwe misa na kwa kuwa amefungiwa upadri watatafuta padri mwingine.
“Kweli Aprili 24 alikuja kwangu na kufanya misa, maneno ninayokumbuka alitaka tupige picha lakini akaniambia itakuwa ya mwisho.
“Maneno yake yalinifanya nikatae baada ya kusema ndiyo picha ya mwisho, nikawa najiuliza mwisho huo ni mimi au yeye padre. Kwa kuwa nilishindwa kupiga naye picha hiyo, leo nitapiga naye hapa akiwa amelala kama kumbukumbu yangu,” amesema.
Amesema maagizo aliyomuachia ni kufanya misa na Mama Maria Nyerere, ambaye ameeleza alikubali lakini Padri Nkwera ameondoka kabla haijafanyika.
Dk Nchimbi amesema ameuliza wasaidizi wake kulikoni, wamemjibu kama Mama Maria yupo tayari itaendelea naye amekubali. Mama Maria alishiriki katika misa kumuombea Padri Nkwera. Pia alikuwapo Mwingine aliyekuwapo mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda.
Kuhusu mchango wa Padri Nkwera amesema alikuwa na sala 30 za kuiombea nchi, akimwelezea kuwa aliheshimu misingi ya Katoliki na hata alipopaswa kufanya misa alitafuta padri mwingine.
“Aliyatii mamlaka ya kanisa kikamilifu na kufuata maelekezo aliyopewa. Hakuna mazungumzo aliyofanya asiguse umuhimu wa amani na umoja kwa nchi yetu.
“Kama ni wosia ametuachia basi ni kuilinda amani ya nchi yetu kama mboni ya jicho letu. Tufanye matendo yanayoongeza umoja wa nchi yetu,” amesema.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema alianza kumsikia Padri Nkwera akiwa mdogo anasoma shule ya msingi, akisimuliwa na baba yake kuhusu sifa zake tatu.
Amezitaja kuwa ni alikuwa padri wa kanisa Katoliki, alikuwa mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na mwenye kipaji na karama ya pekee ya kuombea watu.
“Nilibahatika kuonana naye kwa mara ya kwanza 1988 Tabora, baadaye nilionana naye mara nyingi na ya mwisho mwaka huu, mwezi wa pili.
“Nikiwa safari kaka yangu Laurance Ndumbaro alinitaarifu kifo chake nami nimelazimika kukatiza ziara yangu ili kushiriki sherehe yake hii,” amesema.
Mama mtendakazi wa kituo hicho, Eledina Ntandu, amesema Padri Nkwera alikijua kifo chake mapema, akieleza Aprili 28, 2025 ilikuwa siku yake ya kuzaliwa na alipoiadhimisha alimuita mhandisi anayefanya shughuli za ujenzi katika kituo hicho akimtaka amchoree ramani ya makaburi manne, moja likiwa lake na kuandika maelekezo akiomba akifa azikiwe hapo.
“Ni kutokana na hilo hata mafundi leo (Mei 17) katika kuchimba kaburi lake wamefuata maelekezo aliyoacha. Kwa upande mwingine mtu wa Mungu unapoitwa Mungu anakujalia unajua. Ndiyo maana baba kila kitu alijiandaa, ikiwamo kuchora makabauri kwa mkono wake,” amesema.
Katika mazishi hayo, waumini wameandika maombi ya wenye uhitaji, changamoto za miili na roho.
“Baba yapokee yote, yafikishe huko unakokwenda, ninaamini kilichoandikwa ndani ya bahasha hizi na makarasti haya, kilichopo ndani ya mioyo yao ninaamini maombi ya watoto hawa yamekwisha kupata kibali cha Mungu.
“Ulisema nisiende mikono mitupu, ulisema wanitume maombi yao na nina kukabidhi yote baba kama ulivyoomba,” amesema Ntandu, kisha maombi hayo yaliyokuwa kwenye bahasha na karatasi yaliingizwa kwenye kaburi la Padri Nkwera.
Amesema kazi aliyoifanya Padri Nkwera ilikuwa na mambo mawili; aliponya roho za watu na alikuwa mtumishi wa Serikali.
“Pamoja na kuwa mwalimu alikuwa ni mkaguzi wa elimu, ni msomi hakuwa mbumbumbu. Alikuwa na digrii zake mbili za utawala na lugha. Ndiyo maana aliandika vitabu vingi vya kuielimisha jamii na vya Mungu,” amesema.
Ntandu amesema alikuwa mshauri mzuri, alisaidia kila mtu ndiyo maana watu mbalimbali wakiwamo viongozi walifika kuomboleza.
Ametaka aliyoyahubiri yatumike kumuenzi kwani hata viongozi wa Serikali aliwataka wawe waaminifu na kuliomgoza Taifa kulingana na maadili ya Kimungu.
Mwenyekiti wa huduma za maombezi wa kituo hicho, Deogratius Karulama akisoma wasifu wa Padri Nkwera amesema alizaliwa katika Kijiji cha Lifua, Parokia ya Luilo wilayani Ludewa mkoani Iringa, mwaka 1936.
Aliwahi kufanya kazi Wizara ya Elimu na Utamaduni akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora akifundisha Kiswahili kidato cha kwanza, cha pili, cha tano na cha sita mwaka 1973 hadi 1979.
Karulama amesema mwaka 1979 hadi 1994 Padri Nkwera alikuwa mkaguzi wa shule Kanda ya Magharibi (Tabora na Njombe) hadi alipostaafu mwaka 1995. Wakati huo pia alikuwa akitoa huduma za kuombea watu.
Msanii wa kughani mashairi, Mrisho Mpoto aliwatoa machozi waombelezaji katika shughuli za mazishi alipoelezea wasifu wa Padri Nkwera.
Moja ya sehemu iliyowaliza ni pale alipohoji wapi waanzie kuhusu Padri Nkwera, kule kwao alipozaliwa kwa mama yake, kanisani alipotengwa.
Akizungumza na Mwananchi, Mpoto amesema Padri Nkwera amechangia katika sanaa yake kwa kuwa alikuwa akisoma vitabu vyake vya Kiswahili.
“Huyu kachangia sanaa yangu, nimesoma vitabu vyake vingi vya Kiswahili alivyoandika ambavyo vimenisaidia kughani mashairi. Moja ya jambo alilokuwa akisema si lazima kwenye kuandika mashairi maneno yaendane ndiyo maana hata leo mimi naweza kuimba kutokana na tukio litakalokuwa mbele yangu kwa wakati huo,” amesema.
Hata hivyo, amesema anasikitika hajawahi kughani mashairi mbele yake mpaka leo alipohudhuria msiba licha ya kuwa walikuwa wanazungumza naye mara kwa mara kwa njia ya simu.
Amesema anakumbuka Padri Nkwera aliwahi kumuasa kutotanua mabega kutokana na mafaniko, wala kuonyesha vile alivyopata zikiwamo mali kupitia mafanikio hayo.
“Nakumbuka aliwahi kuniambia wewe leo unaonyesha ghorofa ulilopata kwa ajili ya sanaa yako, wakati huohuo kuna mtu analala chini, tena nje unadhani anajisikiaje anapokuona,” amesema.