Polisi walivyojitofautisha, Lissu akiletwa Kisutu

Dar es Salaam. Licha ya matarajio ya wengi kuhisi hekaheka za Jeshi la Polisi zitaongezeka mara dufu katika kuimarisha ulinzi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu ameletwa ambako kesi zake zinaunguruma, hali imekuwa ni tofauti.

Jeshi hilo licha ya kuimarisha ulinzi, halitumii nguvu kubwa kutawanya wananchi kama ile iliyotumika kipindi cha nyuma ambapo kesi hizo zilikuwa zikisikilizwa kwa mtandao bila Lissu kuletwa mahakamani hapo.

Polisi hao kwa leo wamekuwa wakizungumza kwa utulivu na wafuasi wenye sare za Chadema ambao wako umbali wa kama mita 100 kutoka geti la Mahakama hiyo.

Awali Polisi hao walitaka wanachama hao waondoke, wakawagomea kwamba wao hawafanyi vurugu na wameruhusiwa kuja eneo hilo na kutaka waachwe kwani wamekubaliana kuingia mahakamani kwa zamu.

Gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop wakati likiwasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam likiwa limembeba Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu leo Jumatatu Mei 19, 2025. Picha na Michael Matemanga

 “Sisi hapa hatuvunji sheria na hatutoki, tumeruhusiwa kuja mahakamani,” walisema wafuasi hao na polisi kuwaomba warudi nyuma, lakini ombi hilo lilishindikana.

Wakati hayo yakitendeka, ndani ya Mahakama kesi hiyo ilikuwa ikiendelea huku Polisi 16 wenye silaha wakiwa wamezunguka geti hilo kuimarisha ulinzi, huku wengine kadhaa wakizunguka maeneo tofauti jirani na Mahakama hiyo.

Raia wanaruhusiwa kupita na mara kadhaa Polisi wakiwaelekeza, tofauti na nyakati za nyuma ambapo walitumia mbwa kutawanya raia  na kuzuia watu kusimama pembezoni wakiwatawanya kwa mbwa, jambo ambalo leo halipo.

Itakumbukwa siku za  nyuma kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa, jeshi hilo halikuruhusu raia yoyote kusimama jirani na eneo hilo na kuwafukuza kwa mbwa.

Leo imekuwa ni tofauti, achilia mbali raia wapita njia, Polisi wanawasikiliza wafuasi wa Chadema waliopo eneo hilo na kuzungumza nao bila kutumia nguvu, huku mara kwa mara wafuasi wakihoji ubaya wa wao kusimama eneo hilo na Polisi kuwajibu bila kutumia nguvu.

Lissu ambaye yupo rumande Gereza la Ukonga, anakabiliwa mashitaka matatu la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma kinyume cha sheria ya makosa ya kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Katika shitaka la kwanza, Lissu anadaiwa kuchapisha maneno yanayosomeka: ” Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Raisi, wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na ya kupotosha umma.

Shitaka la pili anadaiwa kuwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na za kupotosha umma kuwa:

“Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi’.

Katika shitaka la tatu anadaiwa kuwa siku hiyohiyo alichapisha taarifa kuwa:

“Majaji ni MA-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Lissu anakabiliwa na shitaka hilo, kinyume na kifungu cha  39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3,2025 ndani ya jiji la Dar es Salaam, ambapo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi  Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuandika maeneo yafuatayo.

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kwa mara ya kwanza, Lissu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, 2025 na kusomewa kesi hizo.