Kigaila: Tunafunga ukurasa rasmi wa kuizungumza Chadema, ni Chaumma

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila amesema baada ya kuwapokea vigogo 3,000 waliokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wataanza kuweka mikakati rasmi ya kupambana na adui wao wa kudumu. Wamemtaja adui huyo kuwa ni Chma cha Mapinduzi (CCM).

Kigaila amesema mipango yao nikufunga ukurasa wa  kuacha kuijadili Chadema na kujikita kukijenga Chaumma na kuwa chama kikubwa kushinda vyama vingine vyote 19 vya siasa Tanzania ikiwemo CCM wanaoshika dola.

Hayo ameyazungumza Leo Jumatano, Mei 21,2025 wakati anafanya mahojiano na Mwananchi kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza kunakoendelea hekaheka za kuwapokea wanachama zaidi 3,000 waliokihama Chadema na kujiunga na chama hicho tayari kwa kujipanga na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Kigaila aliyetunukiwa wadhifa huo muda mchache baada ya kujiunga na chama hicho Mei,19, 2025 katika Ukumbi wa Golden Tulip Masaki jijini hapa, amesema wanafunga ukurasa wa kuwazungumza Chadema kwa kuwa hawakujiunga na chama hicho kushindana na chama hicho.

“Tunataka kufunga ukrasa rasmi wa kuizungumzia Chadema leo baada ya kuwapokea hawa makada 3,000 na kuanza kupambana na adui wetu wa kudumu CCM, tuliihama Chadema kwa sababu ambazo tulishasema hatuwezi kurudia tena kuzisema,” amesema Kigaila.

Kwa mujibu wake, wamejiunga kuendeleza malengo yao na kukiacha Chadema ambacho anadai kwa muda mrefu walikuwa wakitengwa na kubaguliwa kwenye mambo muhimu ya kufanya uamuzi wenye maslahi kwa chama.

“Sisi timu yetu ambayo imeingia Chaumma itaacha na kufunga ukurasa wa kuijadili Chadema na tutaelekeza nguvu zetu kwenye malengo mapana ya kupigania haki za Watanzania na wale wanaotaka kutujadili, wao tunawaacha waendelee tu kwa kuwa hawana ajenda, lakini kwetu tunataka kuonyesha tunajua kufanya kazi na si kubwabwaja,” amesema Kigaila.

Amesema mipango yao ni kushindana na CCM huku akisema hawawezi kupoteza muda kukabiliana na Chadema kwa sababu hawana madaraka yoyote ya kutaka kuwanyang’anya.

“Chadema ana nini ili tukamnyang’anye, chama cha siasa malengo yake ni kushika dola na inashikiliwa na CCM, tunataka tuwafungie kazi, ingawa wanatuita siye madalali basi watuache kama tumenunuliwa tumewacha wakae wao kama marafiki, tunaenda kuendeleza tulipoishia Mlimani City kuwapigania Watanzania,” amesema.

Kigaila aliyekuwa anashikilia wadhifa kama huo Chadema kabla ya kukoma Januari 2025 baada ya kufanyika uchaguzi mkuu, amesema amefanya mengi ambayo anaamini hatakuondoka kwake ataendelea kupigiwa mfano.

“Mtu aliyefiwa hasemi shida yake ya kufiwa, wanamsemea watu wengine, kwa hiyo mimi ukiwauliza Chadema wenyewe watasema wanajua hakuna aliyejenga Chadema kama mimi pamoja na wenzangu. Nimekaa porini miaka 21 kukijenga chama kuanzia ngazi ya msingi,” amesema Kigaila.

Alipoulizwa kama ni hivyo ilikuwaje akihame chama alichokijenga kwa miaka mingi katika majibu yake amesema; “Chama si gereza na wala si baba wala mama, sema huwa kinaanzishwa na watu wanajiunga na wanaweza kutoka kama kinaacha malengo yake  ya kuanzishwa kwake, kwa wale wenye akili kama mimi na wengine hatuwezi,” amesema.

Amesema watu wenye akili timamu na hawana uchawa wanakiacha kama chama kimepoteza malengo yake ambayo kushika dola lakini hutaki kwenda huko na huna mkakati wa kuzuia uchaguzi.

“Chaumma kitakuwa chama kikubwa sana hawa watu unaowaona hapa wako mikoa yote na majimbo yote Tanzania, waliokuja hapa ni viongozi tu baada ya kuwapokea wanachama tutaanza kwenda kuwapokea mikoani,” amesema.

Kigaila amesema baada ya kumaliza shughuli ya kuwapokea makada hao, Chadema itaendelea na kubaki na viongozi pekee lakini wanachama wote wanatarajia kuwakusanya wawafuate.

“Chama ni wanachama wako hapa, viongozi waliko hapa ni zaidi ya 4,000 na siwezi kujua waliko huko mtaani, tukimaliza mkutano wa leo tutazungumza, lakini mjue adui yetu mkubwa ni CCM na yajayo yanafurahisha,” amesema Kigaila.

Pia amesema baada ya kuwapokea, watapanga ratiba na kuanzia Juni Mosi, 2025 wanaanza ziara mikoani kukijenga chama hicho.

Wakati akieleza hayo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Hashimu Rungwe amesema shughuli inayofanyika katika ukumbi huo ni mwanzo na mafuriko yanakuja kuanzia mwezi ujao huko mikoani.