Mbunge akerwa wanafunzi kusimama katika mabasi

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Juakali amesema kumekuwa na changamoto kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao wanapanda kwenye mabasi ya shule ambao kwa mwaka mzima hawajawahi kuketi katika basi.

Akiuliza maswali ya nyongeza leo Alhamis, Mei 22, 2025 katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, Latifa amehoji Serikali haioni haja ya kutoa kauli kwa shule ambazo zinatumia mabasi ya shule ili kuona wanaweza kuwasaidia kwa kuweka msimamizi wa kike ama kiume.

“Pamoja na jitihada mbalimbali bado mmomonyoko wa maadili umeendelea kuwa changamoto katika shule na kuhoji Serikali haioni haja ya kuweka nguvu maalumu sasa kwa kuweka kwa kuandaa walimu wa maadili katika shule nchini,” amesema.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba amesema Serikali imeshaweka maelekezo maalumu kwa kuhakikisha kuwepo kwa msimamizi wa kiume na kike katika mabasi ya shule ikiwa ni kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama katika maeneo yote.

Amesema Serikali inaendelea kuongeza mafunzo kwa walimu na wadau wengine ili kuwajengea uwezo kuhakikisha kuwa wanakuwa salama.

Katika swali la msingi, mbunge huyo amehoji mkakati gani wa kuwalinda wanafunzi mashuleni.

Akijibu swali hilo, Zainab amesema usalama wa wanafunzi ni kipaumbele cha Serikali ambapo mikakati mbalimbali imekuwa ikitekelezwa ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa katika mazingira salama mashuleni.

“Baadhi ya mikakati inayotumika kuwalinda wanafunzi ni kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia kuanzia nyumbani, njiani na shuleni kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema.

Mingine ni mafunzo kuhusu shule salama kwa wadau muhimu wa ulinzi na usalama wa wanafunzi ambapo mwaka 2024/25 yameendeshwa mafunzo kwa walimu 7,451 wa ushauri na unasihi.

Pia Zainab amesema wameendesha mafunzo kwa wakuu wa shule za msingi 17,817, maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata 900, wenyeviti wa kamati za shule 1,980 na wenyeviti wa bodi za shule 580.

Ametaja mikakati mingine ni kuanzisha dawati la ulinzi na usalama wa mtoto.

Aidha, Zainab amesema ngazi ya kijiji na mitaa yameanzishwa mabaraza ya watoto yanayojumuisha wanafunzi wa msingi na sekondari na watoto waliopo kwenye mfumo usio rasmi.

“Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu changamoto zinazowakabili wanafunzi shuleni, njiani na nyumbani ili kuboresha mikakati kuzitatua,”amesema.

Februari 28, 2025, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilitoa waraka wa elimu namba moja wa kuhusu uboreshaji wa huduma ya magari na mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi.

Waraka huo ambao ulisainiwa na Kamishna wa Elimu, Dk Lyambwene Mtahabwa alitaja miongoni mwa maelekezo ni magari hayo kuwa na wahudumu wa kike na kiume.

Related Posts