Waliohukumiwa jela maisha kwa ubakaji, washinda rufaa

Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha na kufuta adhabu ya kifungo cha maisha jela waliyokuwa wamehukumiwa Juma Mayala na Khamis Abdallah, baada ya kukutwa na hatia ya ubakaji wa genge.

Aidha Mahakama hiyo imebatilisha na kufuta adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha waliyokuwa wamehukumiwa Goodluck Faustine na Mnanka Lyoba.

Wote wanne walishtakiwa kwa kosa la wizi wa kutumia silaha na Mahakama ya Wilaya ya Geita, ambapo Juma na Khamis walishtakiwa kwa kosa hilo lingine la ubakaji wa genge ambapo walikutwa na hatia na kuhukumiwa kwa makosa yote mawili.

Tukio hilo lilitokea saa nane usiku, Mei 17, 2016, katika Mtaa wa Mwatulole mkoani Geita ambapo walivunja vioo vya nyumba ya Askari Polisi, WP 7329 PC Martha (ambaye kwenye kesi ya hiyo alikuwa shahidi wa kwanza), ambapo katika nyumba hiyo alikuwa pamoja na mdogo wake wa kike (shahidi wa pili).

Ilielezwa mahakamani kuwa baada ya kuingia walimtishia Askari hiyo kwa mapanga, wakaiba fedha Sh 85,000, simu mbili aina ya Nokia na Huawei, pamoja na televisheni aina ya Samsung.

Ilielezwa mahakamani hapo baada ya kutenda kosa hilo walimchukua shahidi wa pili (jina linahifadhiwa) na kwenda naye umbali wa mita 50, kisha hao wawili wakambaka msichana huyo.

Jopo la Majaji hao walioketi Mwanza ambao ni Zepharine Galeba, Lilian Mashaka na Deo Nangela, waliotoa hukumu hiyo Mei 21, 2025 ambapo walifikia uamuzi huo baada ya kubaini kesi dhidi ya warufani hao haikuthibitishwa bila kuacha shaka ikiwemo utambuzi wa warufani eneo la tukio.

Baada ya kufikishwa mahakamani wote wanne walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu tajwa hapo juu.

Hii ni rufaa yao ya pili ambapo awali waligonga mwamba katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyotupilia mbali rufaa yao ya kwanza.

Warufani wote walikuwa na sababu nane za rufaa ikiwemo kesi dhidi yao kutothibitishwa bila kuacha shaka yoyote, rufaa ambayo iliungwa mkono na Mawakili wa mjibu rufaa (Jamhuri), hasa katika sababu ya nane kuwa shtaka dhidi yao halikuthibitishwa.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Castuce Ndamugoba.

Wakili huyo aliaangazia makosa kadhaa katika ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ikiwemo utambulisho wa warufani eneo la tukio na kuwa upande wa mashtaka ulipaswa kutoa ushahidi kuhusu chanzo cha mwanga na ukubwa wake kutokana na tukio hilo kutokea usiku wa manane.

Amesema shahidi wa kwanza na wa pili ambao walikuwa katika eneo la tukio, hakuna kati yao aliyetaja mwanga uliowawezesha kuwatambua warufani bila makosa.

Hoja nyingine aliyozungumzia wakili huyo ni kuhusu vitu vilivyoibiwa ambapo aliieleza mahakama kuwa kumbukumbu za mahakama zinaonyesha shahidi wa kwanza alieleza siku yake ilikuwa na alama “M” ikiwa ni kifupi cha jina lake.

Hata hivyo shahidi wa tisa E 7719 Koplo Pascal,hakuitambua simu hiyo kwa alama “M” bali aliitambua kwa rangi nyeusi ambapo wakili Ndamugoba alidai kuwa, hakuna uthibitisho wowote kuwa simu iliyotolewa na shahidi huyo wa tisa ndiyo ya Martha.

Alieleza kuwa mlolongo wa utunzaji wa kielelezo hicho tangu kimekamatwa hadi kufikishwa mahakamani haukutolewa hivyo kuna mkanganyiko wa utambulisho wa simu hivyo katika kesi ya wizi wa kutumia silaha haijaweza kuthibitishwa.

Katika hoja ya mwisho, wakili huyo alieleza ilikuwa ni mkanganyiko wa shahidi wa nne, Mwangi Kesena na shahidi wa tisa.

Ameeleza Mwangi aliyedai kununua televisheni inayodaiwa ya wizi kutoka kwa mrufani wa tatu Mei 20,2016 ila katika ukurasa wa 118 wa rekodi ya rufaa, shahidi wa tisa alidai mrufani huyo (Goodluck) alikamatwa mei 19, 2016 hivyo asingeweza kuuza televisheni hiyo Mei 20 kwa sababu alikuwa ameshakamatwa na yuko chini ya ulinzi wa Polisi.

Warufani wote wanne walikubaliana na hoja za Wakili huyo na kuiomba mahakama kuwafutia adhabu hizo na kuamuru waachiliwe kutoka gerezani.

 Baada ya kusikiliza hoja za hizo, Majaji hao walieleza kuwa kuwa wamepitia kwa kina kumbukumbu za rufaa na kuzingatia mawasilisho ya wakili wa Jamhuri ikiwemo kushindwa kueleza mwanga uliotumika kuwatambua warufani eneo la tukio.

Jaji Galeba amesema ni msimamo ulioamuliwa na Mahakama hiyo kwamba  kutiwa hatiani kuhusiana na kosa lililotendwa usiku, au katika hali nyingine yoyote utambulisho unapaswa kuwa sahihi na kuwa Mahakama hiyo imechukulia jambo hilo linapaswa kuthibitishwa ipasavyo.

“Katika kesi hii shahidi wa kwanza n awa pili hawakutaja chochote kinachohusiana na mwanga au ukubwa wa mwanga eneo la tukio. Ni muhimu kwetu kufafanua hoja yetu, hatushikilii kwamba katika eneo la uhalifu hapakuwa na mwanga hata kidogo, au kulikuwa na mwanga hafifu, hapana,”amesema.

“Hoja yetu ni kwamba hakuna ushahidi wowote kwenye rekodi unaoonyesha kuwa mwanga uliokuwa pale, ulikuwa mkali sana kiasi cha kuwawezesha shahidi wa kwanza na wa pili, kumtambua bila makosa yeyote kati ya warufani, tunaungana na wakili kuwa warufani hawakutambuliwa eneo la tukio ,”amesema Jaji huyo.

Jaji Galeba amesema shahidi wa kwanza alidai baada ya wizi huo,alitoa taarifa kwa majirani na polisi, lakini hakueleza kuwa aliwaambia majirani wa aina hiyo au afisa polisi yeyote kuhusu wahalifu hao ila hakuna jirani au afisa wa polisi aliyeitwa kueleza kwamba shahidi huyo aliwaeleza kuhusu tukio hilo.

Jaji huyo amesema katika ukurasa wa 46 wa rekodi ya rufaa, shahidi wa tatu ambaye ni daktari, Patrick Arbogast, alieleza kuwa shahidi wa pili alimwambia alibakwa na watu wasiojulikana.

“Jambo lingine muhimu ambalo kulikuwa na dosari katika ushahidi wa upande wa mashtaka, lilikuwa kuhusiana na utambuzi wa vitu vilivyoibiwa ikiwemo simu na televisheni na kwa kuzingatia mjadala huo hapo juu,tunakubaliana na Ndamugoba na warufani kwamba kesi hiyo haikuthibitishwa bila shaka,” amesema.

Jaji Galeba amehitimisha kuwa wanafuta hukumu zote za warufani wanne katika kosa la kwanza la wizi wa kutumia sialaha na kwa mrufani wa kwanza na wa pili hivyo wanabatilisha na kufuta hukumu dhidi yao.

“Hukumu za kifungo cha miaka thelathini na kifungo cha maisha zote mbili zimetenguliwa, kwa amri kwamba warufani wote wanne watolewe kutoka gerezani na waachiwe huru, isipokuwa kama watakuwa wameshikiliwa kwa sababu yoyote halali,”ameongeza.

Related Posts