::::::::
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe unaoanzia Mwezi Juni hadi Agosti (JJA) 2025.
Katika taarifa hiyo imeelezea mwelekeo wa hali ya joto na upepo unatarajiwa kujitokeza na kutoa ushauri kwa sekta mbalimbali juu ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na matarajio hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a ameeleza kuwa vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai katika baadhi ya maeneo na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, aliendelea kusema kuwa upepo wa wastani unatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi huku vipindi vifupi vya upepo mkali vikitarajiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi kwa kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025.
‘Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma. Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai huku vipindi vya mvua za nje ya msimu vikitarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, ukanda wa mwambao wa pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.’ Alizungumza Dkt. Chang’a
’Aidha, napenda kuwajulisha kuwa Msimu wa Kipupwe 2025 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu’ Amefafanua Dkt. Chang’a.
Akitoa ushauri kwa sekta mbalimbali hapa nchini, Dkt. Chang’a alisema tahadhari za kiafya zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi au vumbi, kwa wafugaji wanashauriwa kutumia maji na malisho