Mawaziri wa Habari na Teknolojia Afrika kujadili utawala wa mtandao

Dar es Salaam. Mawaziri wa Afrika wanaoongoza wizara  kwenye masuala ya habari na teknolojia wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam, katika kongamano la Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF) wakijadili mambo muhimu yanayohusu sera, matumizi, kanuni na mambo mengine yanayohusisha uchumi wa kidigitali.

Kongamano hilo linalotarajiwa kuanza Mei 29 hadi 31, 2025 limetanguliwa na mafunzo kwa kundi la vijana wa Afrika, kujadili sera za intaneti kwa Afrika nzima jinsi gani intaneti itatumika kuwatengenezea fursa Waafrika hasa vijana.

Akizungumza leo Jumamosi, Mei 24, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga amesema kabla ya mkutano mkuu, wameanza na mafunzo hayo kwa wanafunzi 60 kutoka bara la Afrika yaliyoratibiwa na ‘African School on Internet Governance: AfriSIG’.

Amesema wanafunzi hao watajadili sera za intaneti kwa Afrika nzima, jinsi gani itatumika kuwatengenezea fursa Waafrika hasa vijana.

“Kutakuwa na mafunzo mbalimbali yakiangalia namna gani mapinduzi ya kidijitali yanayoletwa na intaneti yanaweza kuwasaidia Waafrika wote kupata fursa, soko la Afrika kuna fursa nyingi hasa biashara ambazo zinafanywa kwenye mitandao zote zinapitia kwenye intaneti.

“Watakavyojifunza, watafuata mbinu mbalimbali kuvijua na namna gani ambavyo nchi mbalimbali zitaweka sera zao vizuri, ili ziweze kuwasaidia vijana kupata fursa mbalimbali,” amesema.

Dk Mwasaga amesema kwa upande wa Tanzania mafunzo hayo ni fursa kwa vijana kujifunza na kwenda kuwafundisha vijana wenzao.

Amesema sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022 vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 34 wapo karibu milioni 23, akisema ni jeshi kubwa na kwamba serikali inataka iwawezeshe zaidi ili wachangamkie fursa zilizopo, zinazoletwa na intaneti hivyo mafunzo hayo ni muhimu.

“Pia kuwa na huo mkutano mkubwa wa siku tatu ni fursa kubwa zaidi kwa kuwa kuna watu wengi watakuja zaidi ya 1,000 kutoka Afrika na duniani kote kujadili kwa pamoja fursa za kidijitali. Kwakuwa tunayasimamia sisi wenyewe tutapata fursa za kujadiliana, kukutana ana kwa ana na wawekezaji wengine, kujifunza kutoka kwao,” amesema.

Mhandisi wa Miundombinu ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba amesema kuanzia Mei 29 kutakuwa na mkutano mkubwa wa intaneti pamoja na teknolojia za habari, utakaofunguliwa rasmi Mei 30 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.

Amesema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujadili masuala nyeti yanayohusu maendeleo ya intaneti na teknolojia habari Afrika.

“Kutakuwa na kikao kitakachoongozwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa pamoja na Mawaziri wengine wa Afrika watakuwa na mjadala mahususi wakiangalia mambo muhimu yanayohusu sera, matumizi, kanuni na mambo mengine yanayohusisha uchumi wa kidigitali,” amesema.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu, kwa mujibu wa takwimu za ITU za mwaka 2024, ni asilimia 38 pekee ya Waafrika wanaotumia intaneti ya uhakika, huku kwa dunia nzima ni asilimia 68. Hii inaonyesha pengo kubwa,” amesema Mhandisi Magomba.

Ameongeza kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kujadiliana kuhusu njia za kuongeza upatikanaji wa intaneti kwa wote, kuondoa tofauti ya matumizi kati ya mijini na vijijini, pamoja na kuimarisha usalama wa mtandao.

Aidha, teknolojia ya Akili Bandia (AI) itapewa kipaumbele, ikizingatiwa mchango wake mkubwa katika kurahisisha kazi na kuongeza ufanisi, hususan katika zama za nne na tano za mapinduzi ya viwanda. “Tunahitaji kuangalia namna bora ya kutumia teknolojia hii kwa maendeleo ya Afrika,” amesema Mhandisi Magomba.

Mkutano huo pia utajadili mahusiano ya kimataifa katika usimamizi wa mtandao, kwa kuzingatia kuwa suala hilo linahitaji ushirikiano wa mataifa yote na si la nchi moja pekee.

Tanzania inatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu, kwa kuimarisha nafasi yake katika majukwaa ya kimataifa ya Tehama, pamoja na kupata ujuzi, mitazamo na ushirikiano mpya wa kimkakati kutoka kwa wadau wa kimataifa.