Serikali yafichua utapeli wa mikopo unaolenga wanawake Zanzibar

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imebaini mbinu mpya za utapeli zinazotumiwa na baadhi ya taasisi binafsi dhidi ya wanawake, ambapo huwapa mikopo kisha kuwanyang’anya sehemu ya fedha hizo, lakini huendelea kuwalazimisha kuzirejesha kwa ukamilifu.

Hayo yameelezwa leo, Mei 24, 2025, katika mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais anayeshughulikia Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma.

Juma amesema kuwa Serikali imebaini uwepo wa taasisi binafsi (hakuitaja kwa sababu za kiuchunguzi) ikiwa imewatapeli wanawake 12 waliokwisha kutoa taarifa kwa Serikali.

Amesema baadhi ya taasisi zimeanza kufanyiwa uchunguzi na vyombo husika kutokana na tuhuma za utapeli dhidi ya wanawake, ikiwemo kuwapokonya fedha walizopewa kupitia mikopo.

Juma amebainisha hayo wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mwakilishi wa Kikwajuni, Nassor Salim Ali, ambaye alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kutokana na kuibuka kwa taasisi binafsi zinazowanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake wanaotafuta mikopo.

“Ni kweli kwamba baadhi ya taasisi binafsi zinazotoa mikopo zimeanza kujihusisha na utapeli wa hali ya juu. Tayari wanawake 12 wamejitokeza na kutoa taarifa kuwa wametapeliwa.

“Mfano, mwanamke anaomba mkopo wa shilingi milioni moja, lakini taasisi hizo humshawishi kuchukua shilingi milioni mbili. Kwa kuwa wengi wao huwa na uhitaji mkubwa wa fedha, wanakubali. Hata hivyo, baada ya kutoka ofisini, hukutana na mtu anayewalazimisha kumpa shilingi milioni moja, hivyo kubaki na nusu ya mkopo waliopokea,” ameeleza.

Amesema kwa uchunguzi unaoendelea wamebaini kwamba anayechukua fedha hiyo ni mmoja wa mameneja wa taasisi hiyo.

“Kwa hiyo jambo hili lipo, linashughulikiwa na uchunguzi ukikamilika, wakibainika taasisi hiyo tutaichukulia hatua, na hiyo fedha iliyochokuliwa watawajibika wao wenyewe, na wanawake hao watalipa kile kiasi walichotumia tu. Niwahakikishie wananchi Serikali italisimamia jambo hili na haki ipatikane,” amesema.

Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, Juma Ali Khatib, amesema licha ya Serikali kueleza kwamba imetoa mikopo, bado wananchi wengi hususani wavuvi wanalalamika kutopata mikopo hiyo.

Waziri Hamza ameongeza kuwa Serikali, kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), imeanzisha programu mbalimbali za mikopo ili kuwawezesha wajasiriamali wengi zaidi kwa haraka, na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa kawaida.

Pia, ZEEA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mikopo (LMS) pamoja na usajili wa vyama vya ushirika, ili kupunguza muda ambao mjasiriamali anasubiri kupata mkopo na kuboresha ufanisi wa utoaji wa mikopo.