Serikali yataka sekta madini kunufaisha Watanzania

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha sekta ya madini inatoa mchango wa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya Mtanzania, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya maendeleo jumuishi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Jumamosi Mei 24, 2025, katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Mavunde amesema kuwa kaulimbiu ya “Madini ni Maisha” siyo ya kimazoea, bali inaashiria mchango wa sekta hiyo katika nyanja zote za maendeleo, ikiwemo kilimo, ajira, viwanda na teknolojia.

“Malengo yetu ni kuona sekta ya madini inabeba maisha ya Mtanzania. Leo hii huwezi kukwepa sekta hii, ni kila mahali kuanzia kwenye simu yako, gari, hadi shambani. Kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama urushaji wa ndege zisizo na rubani na upigaji picha wa ardhi, tunaweza kubaini maeneo yenye miamba yenye maji kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya umwagiliaji. Hii inasaidia kuongeza uzalishaji wa kilimo mara tatu kwa msimu,” amesema Mavunde.

Waziri huyo pia amesema sekta ya madini ina nafasi kubwa katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima nchini. Ameeleza kuwa Tanzania bado ni muagizaji mkubwa wa mbolea licha ya kuwa na rasilimali nyingi zinazoweza kuzalisha malighafi za kutengeneza mbolea hizo.

“Tunayo ‘Mining Vision 2030’ ambayo inalenga kubaini maeneo yenye madini muhimu kama Phosphorus kwa ajili ya kutengeneza DIP, na Nitrogen na Potassium kwa ajili ya NPK. Hii itatuwezesha kuvutia uwekezaji wa viwanda vya mbolea na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mavunde amesema Serikali imejipanga kuirudisha hadhi ya madini ya Tanzanite duniani kwa kuyabrand upya kupitia ushiriki wa kimataifa katika minada na masoko ya madini, sambamba na kudhibiti usafirishaji holela.

“Tanzanite ni madini ya kipekee duniani yanayopatikana Tanzania pekee. Tunataka kuyatambulisha tena kimataifa kama alama ya fahari ya Taifa letu. Tayari tumeanza kushiriki minada ya kimataifa ili kuyaweka kwenye ramani ya ushindani wa madini ya vito duniani,” amesema.

Aidha, Serikali inalenga kuibadilisha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuwa kitovu cha huduma za maabara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara. “Tupo kwenye mazungumzo na taasisi ya GTK ya Finland kuhakikisha tunapata ujuzi na teknolojia ya hali ya juu katika huduma za upimaji wa madini,” amesema Mavunde.

Amesema mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021, hadi asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.

“Kasi ya ukuaji wa sekta ya madini imeendelea kuimarika kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021, asilimia 10.8 mwaka 2022 hadi asilimia 11.3 mwaka 2023,” amesema Mavunde.

Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, mapato ya Serikali kupitia Wizara ya Madini yameongezeka kutoka sh623.24 bilioni mwaka 2021/2022 hadi sh753.18 bilioni mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.8 kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara ya Madini ilipewa lengo la kukusanya Sh1 trilioni. Hadi kufikia Mei 14, 2025, tumeweza kukusanya Sh902.78 bilioni sawa na asilimia 90.28 ya lengo,” ameeleza.

Mavunde ameeleza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania moja kwa moja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Related Posts