Unguja. Wakati mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe akieleza kadhia wanazopata wananchi kwa baadhi ya wawekezaji wa hoteli kuzuiwa kuingia kwenye fukwe zilizopo karibu na hoteli hizo, Serikali imesema ni marufuku kwa mwekezaji yeyote kuwafukuza wananchi hao kwani maeneo ya fukwe ni ya jamii.
Hayo yamejiri barazani leo Mei 24, 2025 baada ya Kombo kutaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wawekezaji hao kuwazuai wananchi wasiende kwenye fukwe na wakati mwingine kufunga njia zinazopita karibu na hoteli hizo.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema kwa mujibu wa sheria ya utalii na sheria ya ardhi maeneo ya fukwe ni kwa ajili ya jamii hakuna mwekezaji yeyote mwenye mamlaka kuwazuia wala kuwafukuza.
Hata hivyo, amemwomba mwakilishi huyo kumpatia maeneo ambayo wananchi wanazuiwa ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.
“Fukwe zote ni za jamii kwa mujibu wa sheria zetu sio za mwekezaji, na hili napenda niseme hapa kwa manufaa ya jamii, tuache dhana kwamba wageni hawataki muingiliano na wananchi, lakini ukweli ni kwamba hawa wageni wanapokuja kutembea wanapenda sana kuingiliana na jamii zetu ili wajifunze utamaduni na mila na hiyo ndio dhana halisi ya utalii na kutangaza utamaduni wetu,” amesema Soraga.
Amesema; “Kama mtu anasema wageni hawataki kuingiliana watawezaje kujua tamaduni zetu, kwa hiyo ni kosa kisheria mwekezaji kumzuia mwananchi kwenda kwenye fukwe kwa mujibu wa sheria ya utalii na ardhi fukwe ni mali ya jamii.”
Kuhusu swali lililoulizwa na mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman lini Serikali itatunga sheria maalumu kwa ajili ya hoteli hizo kusaidia jamii (CSR) zinazozunguka katika maeneo hayo badala ya kubaki kama hisani, Soraga amesema wapo kwenye mchakato wa kutunga sheria ili kuondoa hisani hiyo.
“Kwa hiyo niwaombe wawakilishi mchakato huu wa sheria unaendelea kwahiyo ikija tuwe tayari kuipokea ili kusaidia jamii yetu,” amesema Soraga.
Katika swali la msingi la mwakilishi Kombo, alitaka kujua ni kwa kiasi gani hoteli hizo zinashirikiana na jamii katika maeneo husika ili kuhakikisha maendeleo ya jamii yanapatikana.
Pia, Kwa kuwa jamii hizo hutoa maeneo ya vijiji vyao kujengwa mahoteli hayo, je, ni kiwango gani cha mapato hutengwa kwa ajili ya vijiji hivyo na mwitikio wa wamiliki wa mahoteli hayo juu ya utekelezaji wa dhana ya utalii kwa wote kupitia miradi ya kijamii katika vijiji mbalimbali nchini.
Soraga amesema miradi ya utalii ikiwemo hoteli zimekuwa na ushirikiano mkubwa na jamii zinazowazunguka katika mambo ya kimaendeleo katika jamii hizo na na kusababisha kukua kiuchumi katika maeneo hayo hususan katika huduma za kijamii.
Vile vile, amesema hoteli hizo zimekuwa zikitoa mafunzo kwa wanajamii wa maeneo hayo hatimaye kuwapa fursa za ajira ndani ya hoteli.
“Na mimi naomba kukikiri mbele ye baraza lako kwamba ninaendelea kutia mkazo katika vikao mbalimbali nikikutana na wawekezaji kuihusisha jamii katika mnyororo mzima wa shughuli za kitalii na hili ni suala endelevu,” amesema
Amesema hoteli zimekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii zinazozunguka CS kutoka katika mapato yao ili kukuza ujirani mwema na kuimarisha huduma katika jamii husika.
Amesema kumekuwa na muitikio mkubwa kwa wamiliki wa hoteli za kitalii katika kutekeleza dhana ya utali kwa wote kupitia miradi ya kijamii katika vijiji nchini.
“Wamiliki hao husaidia kuimarisha huduma za kijamii kama vile ujenzi wa vituo vya afya, shule pamoja na kutoa vifaa mbalimbali vya tiba na masomo. Husaidia kuboresha miundombinu ya maji na njia,” amesema.