Hifadhi ya Saanane yavuna Sh1.4 bilioni kwa miaka saba

Mwanza. Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane imekusanya zaidi ya Sh1.4 bilioni kutoka kwa watalii 123, 292 waliotemelea hifadhi hiyo kwa takriban miaka saba iliyopita, ikiwa ni wastani wa zaidi ya watalii 17,000 kwa kila mwaka.

Katika kipindi hicho, jumla ya watalii 119,532 kutoka Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walitembelea hifadhi hiyo ambayo ilikuwa bustani ya wanyama tangu mwaka 1964 kabla ya kutangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 2023.

Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Jenerali Mstaafu George Waitara, wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya malazi kwa watalii ndani ya hifadhi hiyo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saa Nane, Dk Tutindaga Mwakijambile amesema Watanzania 1,006 walitembelea hifadhi hiyo kwa kipindi hicho.

‘’Jumla ya watalii 2,754 kutoka nje ya Mataifa ya Afrika Mashariki (EAC) walitembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane; idadi hiyo itaongezeka baada ya kuanzishwa kwa huduma ya malazi ndani ya hifadhi,’’ amesema Dk Mwakijambile wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Mei 23, 2025.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurunzi wa Shirika la Hifadhinza Taifa (Tanapa) Jenerali mstaafu George Waitara akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa  huduma ya malazi kwenye mahema maalum ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk Totindaga Mwakijambile. Kulia kwa Jenerali Waitara ni Kamishina wa Uhifadhi, Nassoro Kuji. Wengine pichani ni baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Tanapa. Picha na Peter Saramba

Amesema kwa kuanzia, Tanapa imewekeza zaidi ya Sh276 milioni kwenye ujenzi wa mahema matatu kwa ajili ya huduma ya malazi kwa watalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ambayo awali ilikuwa bustani ya wanyama kabla ya kutangazwa kuwa hifadhi mwaka 2023.

Pamoja na utalii wa kuangalia wanyama, aina zaidi ya 110 wa ndege, mawe na miamba, uotoa wa asili na fukwe, vivutio vingine vinavyopatikana hifadhi ya Saanane ni michezo, burudani na fursa ya watu kufanya sherehe ikiwemo kuvalishana pete za uchumba na fungate kwa maharusi.

Ili kuboresha huduma hizo, Dk Mwakijambile amesema Tanapa imetenga zaidi ya Sh33.7 milioni katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2025/26 kwa ajili ya maboresho ya mindombinu ya michezo na burudani ndani ya hifadhi kuvutia watalii zaidi.

Amesema Tanapa pia inawekeza katika matengenezo na ununuzi wa injini kwa boti za utalii na za doria ndani ya hifadhi hiyo ambapo zaidi ya Sh200 milioni imetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Wanyamapori wanaopatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane yenye ukubwa wa ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 2.18 ni pamoja na pimbi, fisi maji, swala pala, pundamilia, nyumbu, digidigi, tumbuli, mbuzi mawe na samba waliofungiwa ndani ya mabanda.

Hifadhi ya Saanane inatoa fursa na eneo la kujipumzisha na kubarizi kwa wageni na wakazi wa Jiji la Mwanza ambalo Kijiografia ni kitovu cha shughuli za kibiashara na kijamii kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jiraninza Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.

Akizundua huduma ya malazi ndani ya hifadhi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Tanapa, Jenerali (mstaafu) George Waitara amesema huo ni muendelezo wa jitihada endelevu za Serikali za kuboresha huduma na miundombinu ya utalii katika hifadhi za Taifa nchini.

“Ubunifu huu wa huduma ya malazi hifadhi utakaoongeza idadi ya watalii na pato la Taifa kupitia sekta ya utalii,’’ amesema Jenerali (mstaafu) Waitara huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza hifadhi za Taifa kwa faida na manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo

Mmoja wa wadau wa utalii jijini Mwanza, Benedict Mongitta amesema huduma ya malazi ndani ya hifadhi ya Saanane ni kilio cha muda mrefu cha wadau na kuupongeza uongozi wa Tanapa kwa mradi huo huku akishauri kuongezwa kwa idadi ya mahema kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kutalii na kulala ndani ya hifadhi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurunzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) Jenerali mstaafu George Waitara akikagua gwaride la heshima aliloandaliwa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Tanapa wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya malazi kwenye mahema maalum ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza. Picha na Peter Saramba

Kamishina wa Uhifadhi, Nassoro Kuji ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono mipango ya shirika katika masuala ya uhifadhi na mazao ya utalii huku akibainisha mikakati kadhaa ya kuongeza mazao ya utalii katika hifadhi zote za Taifa, lengo likiwa ni kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa.

Related Posts