Shinyanga. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amewahimiza wananchi wa Shinyanga kutafakari kwa kina kuhusu mchango wao katika kuleta mageuzi.
Amewakumbusha kuwa kila kura ina thamani kubwa na ni silaha muhimu ya kuleta mabadiliko ya kweli.
Akizungumza leo Jumamosi, Mei 24, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Town School, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, Othman amabye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amewahimiza wananchi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Tushiriki uchaguzi, kwa sababu uchaguzi ni uwanja wa mapambano. Ingawa nguvu kubwa ya dola imetumika kwa jina la mageuzi, matokeo yake ni kwamba nchi imevurugika.
“Ni muhimu tukumbuke kuwa nchi hii si ya mtu binafsi, si ya shangazi wala mjomba, bali ni mali ya wananchi,” amesema Othman.
Naye Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Taifa, Ado Shaib, amesema kuwa ziara ya Mwenyekiti wa chama kwa Kanda ya Ziwa imeanzia Shinyanga.
Ameeleza kuwa kupitia chama chao, wanahitaji wawakilishi wenye misimamo thabiti, wanaojitambulisha kwa uadilifu na uwajibikaji.
“Katika Mkoa wa Shinyanga, tumeugawa kichama katika maeneo mawili, Shinyanga na Kahama. Chama chetu kinahitaji viongozi wenye misimamo thabiti, wanaoweza kusimamia maslahi ya chama bila kuyumbishwa na mtu yeyote.
“Mfano bora wa uongozi wa aina hiyo ni hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyesimama imara katika kupigania uhuru wa nchi yetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mbaluku Haji, ameushukuru umma kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo, akisema kuwa mwitikio huo utakuwa chachu kwa wananchi wengine kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kupigania haki zao.
“Tunashukuru wananchi wa Shinyanga kwa kuitikia wito wa kuja katika ziara hii. Mwenyekiti ametuheshimisha kufungua ziara yake ya Kanda ya Ziwa mkoani Shinyanga katika kuhimiza wananchi kushiriki uchaguzi kikamilifu,” amesema Haji.