Kwa nini mtoto wa mwajiriwa hawi mjasiriamali?

Katika jamii nyingi, kuna mtazamo unaojitokeza mara kwa mara kwamba watoto wa waajiriwa huwa na uwezekano mdogo wa kuwa wajasiriamali wakubwa wanapokua.

Ingawa si sheria ya jumla, kuna sababu nyingi za kijamii, kisaikolojia na kimfumo zinazochangia hali hii. Ukweli huu unapaswa kuchambuliwa kwa kina ili jamii iweze kuhamasisha kizazi kipya kujifunza ujasiriamali, bila kujali aina ya maisha au mazingira waliyozaliwa nayo.

Kwanza, watoto wa waajiriwa hukua katika mazingira ambayo kipaumbele ni ajira yenye uhakika na mshahara wa kila mwezi.

Mara nyingi, wazazi wao huwasisitizia umuhimu wa kusoma kwa bidii ili wapate kazi nzuri, si kuanzisha biashara. Kwa mfano, ni kawaida kusikia mzazi akimwambia mtoto, “soma usije ukahangaika kama watu wa mtaani.”

Hili humjengea mtoto fikra kwamba kazi ya kuajiriwa ndiyo njia salama ya maisha, na kwamba biashara ni ya watu waliokosa elimu au waliokata tamaa.

Pili, waajiriwa wengi hawana mtaji wa kutosha kuwekeza katika biashara. Kwa sababu kipato chao kimepangwa na mara nyingi hakitoshi kuanzisha biashara, watoto wao hawapati fursa za kujifunza vitendo vya ujasiriamali nyumbani.

Tofauti na watoto wa wafanyabiashara ambao hukua wakisaidia biashara za familia, watoto wa waajiriwa hukua katika mazingira ya kutegemea mishahara pekee. Kutokana na hilo, hawana nafasi ya kujifunza mbinu za biashara kama vile kuhudumia wateja, kusimamia faida na hasara, au kufanya uamuzi wa kibiashara.

Aidha, mfumo wa elimu katika nchi nyingi, hasa zinazoendelea, unaelemea zaidi kwenye maandalizi ya wanafunzi kwa ajili ya ajira badala ya ujasiriamali. Mitalaa mingi husisitiza nadharia kuliko vitendo, huku mafanikio yakipimwa kwa uwezo wa kupata kazi serikalini au mashirika binafsi.

Mtoto wa mwajiriwa anapohitimu na kupata kazi, huona kuwa amefikia kilele cha mafanikio, na hivyo hana motisha ya kuanzisha biashara.

Vilevile, hali ya kisaikolojia ya kutaka “usalama wa kipato” ni kikwazo kikubwa. Watoto wa waajiriwa hujifunza kutoka kwa wazazi wao kwamba mshahara ni chanzo salama cha maisha, wakati biashara inaonekana kuwa na hatari nyingi.

Kwa hiyo, hata kama mtoto ana wazo la biashara, anaweza kukosa ujasiri wa kuacha ajira au kujaribu kitu kisicho na uhakika wa mafanikio ya haraka.

Watoto wa waajiriwa si kwamba hawawezi kuwa wajasiriamali, bali hukumbwa na changamoto nyingi za kimtazamo, mazingira na mfumo wa kijamii unaowasababisha kuamini kuwa ajira ni njia bora zaidi ya maisha.

Ili kubadilisha hali hii, kuna haja ya kuanzisha elimu ya ujasiriamali mapema shuleni, kuhamasisha familia kuingiza watoto wao katika shughuli za uzalishaji mapema, na kubadilisha mtazamo kuhusu biashara kama njia halali ya mafanikio ya kiuchumi.

Related Posts