ANTI BETTY: Familia inanilazimisha kuishi na mume niliyemfumania

Anti habari. Naomba unisaidie kuishauri jamii kuhusu kumlazimisha mwanamke kuishi na mwanaume asiyekuwa mwaminifu.

Nimemfumania mume wangu na binamu yake ambaye tumemlea tangu akiwa mdogo.

Huyu binti licha ya kuwa ni ndugu yake ni mdogo mno, hata kujitunza yeye mwenyewe hawezi.

Sijamfumania kwa meseji kwenye simu, hapana kwa kuwaona kwa macho yangu baada ya kutonywa na dada wa kazi kuwa wawili hao wana uhusiano usio wa kawaida.

Niliambia wasiwasi huo tangu miezi mitano iliyopita nikaanza kufanya uchunguzi kimyakimya bila kutaka huyu dada wa kazi ajue suala hilo limenistua na ninalifanyia kazi.

Hatimaye uchunguzi wangu ulizaa matunda baada ya kuwakuta dhahiri shahiri kwenye chumba cha uani, ambacho hutumiwa na vijana wa kiume wanapokuja kututembelea hapo nyumbani.

Nahisi huwa ananiwekea dawa ya usingizi kwenye kinywaji, kwani huwa naziona hekaheka zao kama wanasubiri niage nakwenda kulala, kisha nikiingia ndani mwenzangu huja na kinywaji kama siyo soda ni maji na kunipa ninywe nami hunywa kama kurudisha mapenzi anayonionyesha kwa kunijali kuniletea kinywaji bila kumuomba.

Sikuona dalili za kuwekewa dawa, ila nilikuwa ninalala usingizi mnono bila kushtuka hadi asubuhi, siku hiyo aliniletea soda, lakini sebuleni kulikuwa na mechi timu za nje zilikuwa zinacheza na alikuwa anafuatilia kwa karibu, hivyo alivyonipa akaondoka, nikapata wazo ngoja nimwagie chooni nione nitalala kama siku mbili hizi.

Alipokuja ndani nikajifanya nimelala, akaniangalia kujiridhisha kisha akavaa pensi akatoka ndipo nikamsaka kila mahali nikaja kuwakuta huko bandani hawana wasiwasi wanajua nimelala.

Nina ushahidi wote mpaka picha na video. Cha kushangaza nilipokwenda nyumbani ndugu zangu wameitisha kikao na wamenikomalia nirudi nyumbani nikalee watoto. Ili kuficha hiyo aibu huyu ndugu yake niendelee kuishi naye.

Nivumilie kwa hadithi ndefu, ila naona kabisa sina maisha maana moyo wangu hautaki ila ninalazimishwa. Naomba utoe ushauri kuhusu athari za uamuzi wa wazazi na kulazimishana kurudi kwenye ndoa inayoua kimyakimya kama hii yangu. Maana ninalazimishwa kuishi na watu walioniendea kinyume.

 Pole sana, ila jamii inabidi ijifunze uamuzi kama huu waliouchukua hauna afya kwani mnaweza kuja kudhuliana siku moja.

Kumlazimisha mwanamke kuendelea kuishi na mume wake ambaye amemfumania na ana uhusiano na mdogo wake kunaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya yake ya akili na hatokuwa na heshima kwenye jamii kwani duniani hakuna siri ya watu wawili, lazima watu watajua kila kilichotokea na kumdharau.

Pia inaweza kusababisha msongo wa mawazo, huzuni, na kukosa amani ya akili kwa mwanamke huyu, kwani anahisi kuwa haki yake haijaheshimiwa na anabeba mzigo wa kuishi kwa masharti.

Pili, kuishi katika mazingira yasiyo na uaminifu kunaongeza hatari ya kuwapo chuki ya kudumu, hasira na kuhisi kudharauliwa, hii inaweza kuathiri kinga za mwili na kumsababishia maradhi ya mara kwa mara na hata kudhoofika mwili.

Hao watoto anaotakiwa akawalee pia hawatakuwa na maadili mema wakipata habari ya namna hii. Watakuwa wakijua kutembea na ndugu ni kosa dogo linaloweza kumalizwa kwa kikao cha familia kinachomkandamiza mwingine na kumpa nafasi dhalimu mwenye nia ovu.

Ndoa ni maelewano siyo kuumizana, familia msiwe sababu ya wengine kuumia kwa kisingizio cha watoto.

Related Posts