Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki alisema Afrika haikabiliwi na changamoto ya sera bora, bali inakumbwa na tatizo la ombwe la watekelezaji wa sera hizo kwa manufaa ya watu wake.
Katika hoja yake hiyo, alisema kuna umuhimu kwa bara hilo, kuzalisha rasilimali watu itakayomudu utekelezaji wa sera hizo na hatimaye Afrika inufaike na rasilimali zake.
Wakati huohuo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema uwekezaji katika ujuzi wa watu wa Afrika, utawawezesha kuzitumia na kusimamia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya kiuchumi wa bara lote.
Mbeki aliyasema hayo jana Jumamosi, Mei 24, 2025 alipohutubia mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika, uliofanyika katika Kituo cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Mbeki alisema Afrika ina sera nzuri kwa ajili ya kesho yake, lakini tatizo ni uhaba wa wenye uwezo wa kuzitekeleza ili zikawe na manufaa kwa bara lote kwa ujumla.
Alisema ni muhimu sasa Afrika kuhakikisha inatengeneza rasilimali watu kwa ajili ya utekelezaji wa sera hizo ili zikalinufaishe bara hilo.
Sambamba na hayo, alisisitiza umuhimu wa Afrika kuwa na ujuzi wa kutosha wa ndani, ili kuepuka utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya bara husika.
Hata hivyo, alisema bara hilo lina wasomi na wataalamu wa kutosha kushughulikia changamoto zinazolikabili bila kutegemea usaidizi kutoka nje.

Mbeki alisema licha ya juhudi mbalimbali zilizofanyika alipokuwa madarakani, sasa ni wakati wa sekta binafsi Afrika kuongoza kuunda ajenda ya kiuchumi ya bara hili kimataifa.
“Lazima tuwe na mpangilio na kuzungumza kwa sauti moja kuhusu masuala ya msingi,” alisema huku akiwakumbusha kushindwa kwa Mpango wa Utekelezaji wa Afrika (Africa Action Plan) katika miaka ya nyuma, akitoa wito wa kuandaa mapendekezo ya sera yatakayoongozwa na Waafrika.
“Tulikuwa na juhudi kadhaa katika mikutano ya G8 kushinikiza ajenda ya maendeleo ya Afrika kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe. Sasa, kwa kuwa Umoja wa Afrika ni mwanachama wa G20, tunapaswa kutumia fursa hii kusukuma mbele ajenda yetu,” aliongeza Mbeki.
Kwa upande wake, Mchumi mashuhuri Profesa Samwel Wangwe alisisitiza hitaji kwa mataifa ya Afrika kurejea katika misingi ya kujitegemea na kutathmini upya nafasi ya Umoja wa Afrika.
Alipendekeza pia kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja, ulinzi wa rasilimali asilia, uwekezaji katika ujuzi wa ubunifu wa kibiashara, na kuweka mazingira rafiki kwa ukuaji wa uchumi kupitia ushirikiano thabiti kati ya sekta ya umma na binafsi.
Alichokisema Profesa Kabudi
Akishiriki moja ya majopo katika mhadhara huo, Waziri wa Habari, Kabudi alisema kuna haja kwa Afrika kuimarisha taasisi zake, uchumi, miundombinu, utawala wa sheria na sekta nyingine muhimu.
Kufanya hivyo, alisema kutachochea ufanisi kwa Serikali, kadhalika kuhakikisha ustawi wa maendeleo ya wananchi.
Wakati hayo yanafanyika, alisema ni muhimu wananchi washirikishwe kwa kila hatua, ili nao wawe sehemu ya washiriki wa kuyafikia malengo kusudiwa.
“Wananchi wanaweza kushiriki kwa mawazo, ujuzi, ubunifu na namna nyingine zitakazowezesha kufikiwa kwa malengo yetu kama Afrika,” alisema.
Kutokana na rasilimali zilizopo, Profesa Kabudi anaona ni muhimu Afrika iwekeze katika ujuzi kwa watu wake, ili wawe na uwezo wa kuzitumia na kusimamia kwa manufaa ya kiuchumi wa bara lote.
Uwekezaji katika teknolojia ni jambo lingine lililotajwa na mwanazuoni huyo kama mbinu ya kuiinua Afrika kwa kile alichoeleza, utatanua wigo wa mafanikio ya sekta nyingine.
Sambamba na hayo, alisema bara hilo linapaswa kudumisha utawala wa sheria kwa kuanza kuifanyia mageuzi bodi ya ushauri kuhusu masuala ya rushwa, ili iwe taasisi imara inayowajibisha.
“Napendekeza kwa Rais wangu Samia Suluhu Hassan kuifanya bodi ya masuala ya rushwa isiishie kuwa ya ushauri badala yake iwe na nguvu ya kusimamia na kuhamasisha uwajibikaji,” alisema.
Wakati Profesa Kabudi akiyasema hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema ni bahati mbaya mataifa ya Afrika yanazungumzia umoja kwa nadharia.
Kiuhalisia, alisema mataifa hayo hayana umoja na hayajaunganika kama inavyozungumzwa, akitolea mfano safari yake kutoka Dar es Salaam kwenda Luanda nchini Angola ilivyochukua takriban saa 18 kupitia Afrika Kusini, ilhali ilipaswa kuchukua saa tatu pekee.
“Hili ni miongoni mwa mambo tunayopaswa kuyatatua, kwamba kwa nini hatujaungana,” alisema.
Katika hotuba yake hiyo, alisema hivi karibuni alikwenda Afrika Kusini kuwatembelea watu kadhaa waliokwenda kwa matibabu na alitembelea kituo bora cha tiba nchini humo, huku akijiuliza kwa nini watu wa Afrika wanakwenda kutibiwa nje ya bara hilo.
“Nafikiri Mzee Mbeki na wanajopo haya ndio mambo tunayopaswa kuyajadili. Tumezungumza sana kuhusu umoja lakini hatujui thamani yetu, mmoja nje ya Afrika anajaribu kuonyesha thamani yake,” alieleza.
Aligusia uchumi wa buluu, akisema Tanzania Ina fursa nzuri za uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu visiwani Zanzibar, lakini hakuna nchi ya Afrika iliyopeleka hata boti moja kutumia fursa hiyo.
Alieleza unapozungumzwa usalama wa chakula ni vema kutafakari kwa nini Afrika inashindwa kukitosheleza na inakuwaje mataifa yenye majangwa yanaingiza zaidi chakula Afrika kuliko nchi za Afrika zenyewe.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, alisema mwaka 1986 wakati wanamshawishi Mwalimu Nyerere kusherehekea mwaka wake wa 76 wa kuzaliwa, aliwaambia kwa nini washerehekee kuzaliwa kwake badala ya kufanya hafla za kutatua na kutafuta majibu ya changamoto za Afrika.
Butiku alisema MNF na Taasisi ya Thabo Mbeki kuanzia sasa zinapaswa kufanya kazi pamoja na kwamba angalau taasisi hizo zinatakiwa kukusanya vitabu vyote vya waasisi wa mataifa ya Tanzania na Afrika Kusini ili kuvihifadhi.
Alisema hazipaswi kuishia tu kufanya kazi pamoja, bali ziendelee kushirikiana popote katika mambo yote kwa sababu zote zinafahamu namna waasisi hao walivyofanyia kazi Afrika.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Unisa), Profesa Puleng Lenkabula alisema kwa kadri siku zinavyokwenda, mihadhara ya Siku ya Afrika imegauka kuwa jukwaa muhimu la majadiliano ya masuala mbalimbali ya kitamaduni na kihistoria yenye masilahi ya bara kwa ujumla wake.
Alisema chuo hicho kinaendeleza jukumu lake la kuhakikisha linaifanya Afrika kuwa bara lenye ujuzi na uchumi na kwamba kimekuwa kikishirikiana na vyuo vingine barani humo na kinachochea maendeleo.
Alisema chuo hicho kimesaini hati ya makubaliano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa ajili ya ushirikiano kwenye maeneo ya taaluma, utafiti na mipango.
Ushirikiano wa Unisa na Taasisi ya Thabo Mbeki, alisema umekuwa msingi wa kulinda historia ya Afrika na utamaduni wake na wanaamini hata Taasisi ya Mwalimu Nyerere inatekeleza hilo.
“Tunapaswa kufanya kazi kwa bidii kujenga kesho yetu. Tumekutana kutathmini tunakokwenda na angalau tujue hatima yetu kama Waafrika,” alosema.