Kiama wanaopangisha wachimbaji wadogo | Mwananchi

Dar es Salaam. Serikali imeamua kuja na mwarobaini wa kupunguza migogoro katika sekta ya madini inayohusisha wamiliki wa leseni za uchimbaji  na wachimbaji wadogo.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari  jijini Dar es Salaam kuhusu miaka minne ya mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya madini, Waziri wa Madini, Antony Mavunde,  amesema baadhi ya waliopewa leseni hawachimbi bali huwakodisha wachimbaji wadogo.

“Huyu mtu mwenye leseni baadaye akipata mwekezaji anataka Serikali kwenda kuwaondoa  wachimbaji wadogo wenye maduara kwa kutumia askari wenye mabomu,’’ amesema

Ili kipunguza migogoro hiyo alisema wameweka utaratibu wa kila mmiliki wa leseni kuingia mkataba na wachimbaji, lakini pia akitokea mwekezaji wachimbaji hao walipwe fidia.

Waziri Mavunde amesema imejizatiti kuhakikisha sekta ya madini inatoa mchango wa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya Mtanzania, ikiwa ni sehemu ya ajenda pana ya maendeleo jumuishi.

Amesema  kaulimbiu ya “Madini ni Maisha” haikuwekwa kwa bahati mbaya bali inaakisi nafasi pana ya sekta hiyo katika kuendesha shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

“Malengo yetu ni kuona sekta ya madini inabeba maisha ya Mtanzania. Leo hii huwezi kuikwepa sekta hii- ipo kila mahali, kuanzia kwenye simu, magari, hadi kwenye kilimo. Kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama ndege zisizo na rubani na upigaji picha za kisayansi za ardhi, tunaweza kubaini maeneo yenye miamba ya maji na kusaidia katika uchimbaji wa mabwawa ya kilimo cha umwagiliaji. Hii inaweza kuongeza mavuno hadi mara tatu kwa msimu mmoja,” amesema.

Kuongezeka bajeti ya madini

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka Sh89 bilioni hadi kufikia Sh294 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni ishara ya dhahiri ya dhamira ya Serikali kuboresha sekta hiyo ya kimkakati.

Fedha hizo zinalenga kuimarisha miundombinu ya kisasa ikiwemo ujenzi wa maabara za kisasa, uboreshaji wa Kituo cha Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sekta hiyo.

Mchango wa sekta katika uchumi

Waziri Mavunde amesema mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea kukua, ambapo mwaka 2021 mchango huo ulikuwa asilimia 7.3, mwaka 2023 ukafikia asilimia 9.1 na mwaka 2024 umefikia asilimia 10.1.

Vivyo hivyo, kasi ya ukuaji wa sekta imeongezeka kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi asilimia 11.3 mwaka 2023.

Kwa upande wa mapato ya Serikali, Mavunde alisema yameongezeka kutoka Sh623.24 bilioni mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sh753.18 bilioni mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.8.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, Wizara ya Madini ilipewa lengo la kukusanya sh1 trilioni. Hadi kufikia Mei 14, 2025, tumekusanya Sh902.78 bilioni, sawa na asilimia 90.28 ya lengo,” amebainisha Waziri huyo.

Mbolea na malighafi za viwandani

Akizungumzia mchango wa sekta ya madini katika kilimo, Mavunde amesema Tanzania ni mmoja wa waagizaji wakubwa wa mbolea licha ya kuwa na rasilimali za kutosha zinazoweza kutumika kuzalisha malighafi hizo nchini.

“Kupitia Mining Vision 2030, tunalenga kubaini maeneo yenye madini ya Phosphorus kwa ajili ya kutengeneza mbolea aina ya DIP, na Nitrogen na Potassium kwa ajili ya NPK. Tukifanikiwa kuvutia uwekezaji wa viwanda vya mbolea hapa nchini, wakulima wetu watanufaika kwa upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu,” amesema.

Tanzanite yapewa hadhi mpya

Waziri Mavunde alibainisha kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuirudisha hadhi ya madini ya Tanzanite katika soko la dunia kupitia mikakati ya branding na ushiriki wa masoko ya kimataifa.

“Tanzanite ni madini ya kipekee duniani na yanapatikana Tanzania pekee. Tumejipanga kuyatangaza na kushiriki kwenye minada ya kimataifa ili kuyaweka kwenye ramani ya ushindani wa madini ya vito,” amesema.

Related Posts