Unguja. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said amekemea tabia ya watendaji wakuu wa taasisi wenye choyo na kuwapiga vita waliopo chini yao. Akisema moja ya sifa ya kiongozi ni kutambua mawazo mazuri ya walio chini yake, kuyaunga mkono na kuyatafsiri ili yalete mchango katika taasisi na maendeleo ya nchi.
Zena ametoa kauli hiyo jana Mei 24, 2025 wakati wa tuzo za uandishi wa habari za kitakwimu katika jinsia zilizoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa ZNZ.
“Tunapokuwa na watu wazuri wa kutusaidia kazini kwa nini tunawapiga vita, kwa kweli niwatake sana tuache roho za kuoneana choyo, hii tabia tuiache mara moja haitujengi, ukiwa kiongozi wewe ndio umepewa hiyo fursa kwa wakati huo, taasisi ikifanya vizuri sifa ya kwanza inakuja kwako,” amesema.
Amesema wanatakiwa kutambua mchango wa wasaidia wao kwani hawawezi kufanya kazi zote kwa ufanisi badala yake lazima wawe na mawazo mbadala.
“Kwa hiyo niombe sana ndugu zangu Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, tusiwahofie wasaidizi wetu wenye uwezo, wako pale kusaidia kwa ajili ya kuhakikisha taasisi zinakwenda vizuri, tuwape ushirikiano tuwape rasilimali,
tuunge mkono jitihada zao kwa sababu mafanikio ya utendaji wao ndio mafanikio ya taasisi, mafanikio ya taasisi ndio mafanikio ya nchi,” amesema.
Zena amesema uandishi wa habari wenye msukumo wa kijinsia ni muhimu kwa sasa kuliko wakati wowote ule.
Amesema mwanamke akipata fursa ya uongozi ana uwezo wa kufanya vyema zaidi kwa sababu katika mazingira yake ya kila siku nyumbani ni ya kiuongozi na kibajeti.
“Uongozi wa mwanamke unaanzia nyumbani, kumbuka yeye ndio anapanga bajeti za familia hata akiachiwa fedha za matumizi anajua anapanga vipi, kwa hiyo huyu mwanamke akipata fursa ya kuongoza anakuwa mzuri hata kwenye mipango kwani tayari ameyaishi maisha hayo akiwa nyumbani,” amesema Zena
Amezipongeza taasisi zinazoandaa tuzo hizo kwa nia ya kumuinua mwanamke, hivyo kuzitaka taasisi zingine kuiga mfano huo katika nyanja mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Tamwa ZNZ, Dk Mzuri Issa amesema hiyo ni mara ya nne kuandaa tuzo hizo lengo ni kuhakikisha wanawake wanakuza sauti zao na kutambuliwa kazi wanazofanya ili kujenga jamii yenye usawa.
Kiongozi wa majaji wa tuzo hizo, Dk Abdallah Mohamed amesema zilipokewa kazi 235 lakini zilizoingia kwenye mashindano ni 120 za mitandao ya kijamii, redio na gazeti.
Hata hivyo amesema changamoto walizokutana nazo bado kazi nyingi hazina weledi, hivyo ipo haja ya kutoa mafunzo na kuwasomesha waandishi kufanikiwa.
Pia ametoa ushauri kwa waandaaji badala ya kujikita katika kipengele kimoja cha jinsia ni vyema pia wakaangalia na vipengele vingine kama uchumi biashara mazingira na maeneo mengi zaidi, ili kutoa mwanya kwa watu wengi kushiriki.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Kassim Ali amesema mpango wa kuandaa tuzo hizo una lengo la kuhamasisha matumizi ya takwimu katika uandishi wa habari, na kutoa taarifa zenye ushahidi wa kisayansi kuthamini na kutambua mchango wa waandishi wa habari.
Tuzo hizo zimeshirikisha waandishi wa mitandao ya kijamii, redio na magazeti ambapo washindi wa redio na mitandao ya kijamii walipata zawadi ya Sh1 milioni na mshindi wa gazeti alipata Sh1.5 milioni huku vyombo vya habari vilivyofanya vizuri vikipata Sh2 milioni.