Balozi Shio agusia suala la amani Afrika

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Innocent Shio amesema licha ya changamoto ya vitisho vya ugaidi na ukosefu wa utulivu katika baadhi ya nchi za Afrika, juhudi zinaendelea kufanyika kuhakikisha amani inarejea.

Balozi Shio ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Mei 25, 2025, katika mbio maalumu za kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, yakihusisha zaidi ya washiriki 1,000.

Baadhi ya nchi ambazo zinapitia migogoro ya kisiasa hivi sasa ni Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia pamoja na Chad

“Tutaendelea kusimamia malengo ya waasisi wa mataifa yetu ya Afrika ili bara letu liwe na amani maadhimisho haya yanatupa nafasi ya kutafakari tulikotoka, tulipo na tunapokwenda,” amesema Balozi Shio.

Balozi Shio amesema lengo la mbio hizo ni kuendeleza mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi wa Afrika, sambamba na kukumbuka historia ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (OAU) mwaka 1963, ambao baadaye uligeuzwa kuwa Umoja wa Afrika (AU).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Hellen Maduhu amesema mbio hizo zinafanyika kwa mara ya pili nchini, awamu ya kwanza ikiwa ni mwaka 2024 ikishirikisha watu 800.

“Mwaka huu tuna washiriki 1,500 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, mbio hizi ni miongoni mwa shughuli tunazofanya kusherehekea siku ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika,” amesema Maduhu.

Kupitia maadhimisho hayo, amesema wamejadili namna ambavyo Afrika inaweza kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Akizungumzia mchango wa mbio hizo amesema huleta watu mbalimbali kujumuika na kushirikiana pamoja.

Mbio za siku ya Afrika hujumuisha umbali wa kilomita 10 hadi 21, ambapo kwa kila kundi, washindi wanne wa mwanzo walipatikana kutoka kwa jinsia ya kiume na ya kike.

Maadhimisho ya siku ya Afrika hufanyika kila mwaka Mei 25 kukumbuka kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) mwaka 1963 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Umoja huo ulianzishwa na mataifa huru 32 ya Afrika kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa bara, kuondoa ukoloni na kukuza maendeleo ya bara zima. Mnamo mwaka 2002, OAU ilibadilishwa rasmi kuwa Umoja wa Afrika (AU).

Related Posts