Moshi. Makada wawili wa Chama cha ACT – Wazalendo, wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya chama chao kugombea ubunge jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Makada hao Livin Msele na Jackson Masawe, wamechukua fomu kwa nyakati tofauti katika ofisi za chama hicho mkoa, zilizopo mtaa wa Kiusa, Moshi mjini huku wakijipambanua kama watakubaliwa, wana uhakika watashinda jimbo hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Profesa Patrick Ndakidemi (CCM).
Akizungumza leo Jumapili Mei 25, 2025 Katibu wa ACT – Wazalendo jimbo la Moshi vijijini, Januari John amesema mbali na makada hao wanaoomba kugombea jimbo hilo, pia yupo Lilian Joseph aliyechukua fomu ya kuomba kuwania nafasi ya viti maalumu.
“Mchakato wa uchukuaji fomu unaendelea na mpaka sasa katika jimbo letu la Moshi vijijini wameshachukua fomu wanachama watatu, ambapo wawili ni jimbo na mmoja ni wa viti maalumu,” amesema John.
Aidha, amesema katika jimbo hilo ambalo lina kata 16, wamejipanga kuhakikisha wanasimamisha wagombea udiwani wenye nguvu na wanaokubalika katika kata zote ili kuweza kupata ushindi.
“Tunatambua uchaguzi ni ushindani na sisi kama chama tumejiandaa na kujipanga ili kwenda kushindana na vyama vingine na Jimbo la Moshi Vijijini tunatambua lina kata 16 ambapo kama chama tunahitaji kusimamisha wagombea udiwani katika Kata zote,” amesema John.
Ameongeza kuwa; “Mkakati mkubwa tulio nao ni kupata wagombea ambao wana nguvu ya ushawishi kwa wananchi na wanakubalika na makundi yote kwenye jamii katika kata na jimbo, tunalenga kupata ushindi katika uchaguzi wa Oktoba.”
Amesema kwa upande wa wagombea udiwani, tayari wamepata watia nia katika kata 10 ambao wamechukua fomu, kata sita kati ya hizo, wametia nia zaidi ya wanachama wawili.
Akilizungumzia hilo, Livin Msele amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya ACT – Wazalendo wakilenga kwenda kuwawakilisha vema wananchi bungeni.
Msele ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Moshi Vijijini, amesema lina changamoto nyingi ikiwemo miundombinu mibovu ya barabara.
Amesema endapo chama chake kitampatia ridhaa ya kugombea, atahakikisha anashinda.
“Nimeona ni muda mwafaka wa mimi kwenda kuwawakilisha na kuwasemea wananchi wa Jimbo la Moshi vijijini bungeni, nimejipanga vizuri na najiamini nitakwenda kushinda endapo chama kitanipa ridhaa ya kugombea,” amesema Msele.