Dar es Salaam. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amesema hali ya kiafya Padri Charles Kitima, katibu mkuu wa Baraza hilo, inaendelea vyema na atarejea katika majukumu yake hivi karibuni.
Padri Kitima alishambuliwa Aprili 30, 2025 na kitu butu kichwani alipokuwa kwenye ofisi za TEC Kurasini Temeke jijini Dar es Salaam na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan.
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilieleza kuwashikilia watu wawili wakishukiwa kuhusika na tukio hilo na kuwa watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Mwananchi limemtafuta leo Jumapili Mei 25, 2025, Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro kujua upelelezi wa tukio hilo ulipofikia, lakini hakupatikana kwani simu yake ilikuwa ikiita bila kupokea na hata ujumbe mfupi aliotumiwa haukupata majibu.
Akizungumza leo kwenye misa ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Josephat Jackson Bududu, Rais huyo wa TEC amezungumzia afya ya Padri Kitima na matumaini yaliyopo.
Misa hiyo imeadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mt. Theresia, Tabora ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, waumini pamoja Serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kama mnavyofahamu aliumizwa, Padri anawashukuru kwa sala, yeye anaendelea vizuri, ni sala na matumaini yetu akiendelea vile atarudi kwenye majukumu yake hivi karibuni.
“Sisi tunaendela kulaani kile kitendo cha aibu, kibaya na kiovu kilicholenga kukatisha maisha ya padri wetu akiwa katika makazi na makao makuu ya baraza baraza.
“Katika utawala bora na wa sheria, wahalifu wale walipaswa wawe wameshafikishwa mahakamani mpaka sasa. Matumaini yetu uchunguzi hautachukua muda mrefu zaidi kabla ya wahusika kufikishwa mbele ya sheria,” amesema ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Lindi.
Ameongeza kuwa ili kuwa na amani, hakuna raia atakayependa kuona wahalifu kama wale uraiani na hakuna raia ambao hawatapenda kuishi katika nchi yao katika amani, haki na ukweli.
“Wala wasingependa kuona magenge kama yale yawe hatari kwetu sisi na kwa watu wengine. Kwa wahusika pia kwa wale wanayoyazalisha, wafahamu makundi kama haya ni hatari kwao, sijui kama wanajua hivyo,” amesisitiza Askofu Pisa.
Aidha amesema: “Tuendelee kuiombea nchi yetu, kuwa na mifumo na sheria nzuri na kulinda raia, amani, haki, kweli na demokrasia,” amesema.
Akimzungumzia Askofu Bududu aliyeteuliwa Februari 26, 2025 na Papa Francis aliyefariki dunia Aprili 21, 2025, amesema historia mpya imeanza leo Tabora kwa kuwa na Askofu Msaidizi.
“Bududu utakuwa msaada mkubwa kwa jimbo kuu la Tabora, TEC na kwa kanisa zima la Tanzania pamoja na jamii inayotuzunguka,” amesema.
Kwa upande wake, Askofu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, amesema Bududu ni askofu wa kila mtu na katika utume wake aendeleze maendeleo ya kijamii bila ubaguzi wowote.
Akisoma hotuba yake kwa lugha ya Kiswahili, Askofu Accattino amesema katika kutimiza wajibu wake wa kuwaongoza watu wa Mungu, Askofu Bududu lazima awe na ushirika na wenzie, umoja pamoja na maelewano.
Waziri Lukuvi akizungumza baada ya misa hiyo, amesema mbali na Rais Samia kushukuru kwa mwaliko huo, ahadi yake ya ushirikiano aliyoitoa kwa Mwadhama Protas Kadinali Rugambwa haijabadilika.
“Kwa wakati wote (Rais Samia) anaendelea kuuishi uhusiano mwema alionao na Kanisa na ataendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa Serikali na wa dini zote,” amesema Lukuvi.