Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump ameeleza kutofurahishwa na mwenendo wa Rais wa Russia, Vladimir Putin kuhusiana na mzozo wa Ukraine.
Akizungumza na vyombo vya habari jana Jumapili, Trump alisema Rais Putin ni mwendawazimu aliyepoteza akili, huku akisema hajafurahishwa na kitendo cha Russia kutekeleza mashambulizi yake nchini Ukraine.
Trump amekuwa akiwatumia wateule wake Keith Kellogg na Marco Rubio kusaka mwarobaini wa mzozo wa Russia na Ukraine tangu aapishwe kuingia madarakani Januari 20, mwaka huu.

“Nimekuwa na uhusiano mzuri sana na Vladimir Putin wa Russia, lakini kuna kitu kimemtokea. Amechanganyikiwa kabisa! Anaua watu wengi bila sababu yoyote, na sisemi tu wanajeshi. Makombora na droni yanapigwa kwenye miji ya Ukraine, bila sababu yoyote.”
“Sifurahishwi na kile ambacho Putin anafanya. Anaua watu wengi, na sijui ni kitu gani kimemtokea Putin,” alisema Trump.
Katika chapisho aliloweka kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump pia alielekeza lawama kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aliyeituhumu Marekani kwa kuwa kimya wakati Russia inatekeleza mashambulizi nchini humo.
Kwa mujibu wa maofisa nchini Ukraine, takriban watu 12 waliuawa katika mashambulizi ya Russia kote nchini Ukraine katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wakiwemo watoto.
Pia kuna maofisa wa serikali na jeshi la Ukraine waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo.

“Dunia inaweza kwenda likizo, lakini vita vinaendelea, bila kujali ni wikendi au siku za kazi. Hili haliwezi kupuuzwa. Ukimya wa Marekani, na ukimya wa wengine duniani unamtia moyo Putin,” alisema Zelensky.
Trump pia aliwaeleza waandishi wa habari kuwa anafikiria kwa asilimia 100 Russia vikwazo zaidi, ambavyo Zelensky amekuwa akivitaka.
Awali, Trump alisema hatashiriki kuiwekea Russia vikwazo vipya kutokana na alichodai kuwa ana imani kutakuwa na nafasi ya kufanya mazungumzo ya kumaliza mzozo huo ndani ya muda mfupi, jambo ambalo haoni matumaini.
“Tuko katikati ya mazungumzo, halafu yeye anarusha makombora Kyiv na kwenye miji mingine,” Trump aliwaambia waandishi wa habari huko New Jersey alipokuwa safarini kuelekea Washington.

Trump, ambaye mara kwa mara amejisifu kuhusu uhusiano wake mzuri na Putin, alizungumza na kiongozi huyo wa Russia Jumatatu katika jaribio la kuanzisha makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 30 kati ya Russia na Ukraine.
Baada ya simu na Putin na mawasiliano ya baadaye na Zelensky na viongozi wengine wa Ulaya, Trump alitangaza kuwa Russia na Ukraine zitaanza mara moja mazungumzo yenye lengo la kusitisha mapigano na vita hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Russia haijatoa kauli yoyote kuhusiana na madai hayo ya Trump.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.