Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa ametoa onyo kwa wageni wanaotaka kuingia nchini wakiwa na nia ya kuchezea amani ya nchi na kwamba watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 26, 2025 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema pamoja na kuwepo jitihada ya kuvutia wageni kutoka nje ya nchi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuvutia uwekezaji, kumekuwa na wageni wachache au kundi wanaopanga kuingia nchini kwa nia ovu ya kuhatarisha usalama na amani.
“Wageni waovu hawana nafasi hapa nchini kwetu, naipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa utimamu wao katika kudhibiti wageni haramu wa aina niliyoitaja na wale wageni wanaoingia nchini kwa kibali fulani na wakishaingia katika jamii yetu, wanafanya mambo kinyume na kibali walichopewa,” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza hayo zikiwa zimepita wiki chache tangu wanaharakati na wanasheria kutoka Kenya na Uganda kuzuiliwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na kisha kurudishwa nchini kwao.
Wanaharakati hao ni Martha Karua (mwanasheria na mwanasiasa wa Kenya) na Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga. Viongozi hao wa zamani wa Kenya walikuja nchini kusikiliza kesi ya uhaini na uchochezi zinazomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Mbali na wanasheria hao, pia, wanaharakati wengine kama Boniface Mwangi wa Kenya na Agather Atuhaire kutoka Uganda, pia walirudishwa kwao baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa na Mamlaka za Tanzania.
Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kushikamana na kulinda nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje, akisisitiza kuwa adui wa Taifa katika karne ya 21 si lazima atumie vifaru bali anaweza kutumia njia nyingine zenye madhara makubwa kwa jamii.
“Adui wa nchi yoyote, ikiwemo yetu, katika karne hii ya 21 si lazima aje na vifaru ndipo ahesabike kuwa ni mvamizi. Anaweza kuja kwa njia ya magenge ya wanaharakati wenye ajenda ya kuvuruga amani kama tulivyoshuhudia hivi karibuni,” amesema Bashungwa.
Amesema Serikali haitakubali kuona amani na utulivu wa nchi vikihujumiwa, na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi salama kwa raia wake.
“Ndugu Watanzania wenzangu, hatutakubali kamwe kuvurugwa. Tutaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kulinda amani na utulivu wa Taifa letu,” amesisitiza Bashungwa.