Wawakilishi waikalia kooni Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameikalia kooni Bodi ya Mikopo Zanzibar kwa kuchelewesha fedha za kujikimu kwa wanafunzi licha ya kutengewa kiasi kikubwa cha fedha.

Wamesema hali hiyo inasababisha wanafunzi kukosa utulivu kwenye masomo yao.

Wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwenye Baraza la Wawakilishi mjini Unguja, leo Jumatatu, Mei 26, 2025, wajumbe wa baraza hilo wameitaka bodi hiyo  kama inashindwa kutekeleza wajibu huo kwa wakati, ni bora fedha hizo kutoka serikalini zikaondolewa.

Katika bajeti ya mwaka 2025/26, programu ya elimu juu imetengewa Sh157.267 bilioni kwa ajili ya kutoa elimu itakayomwezesha muhitimu kujiajiri au kuajiriwa.

Mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe amesema wanafunzi wanalalamika, wanapitia wakati mgumu vyuoni kisa kuchelewa kuingiziwa fedha za kijikimu, hivyo bodi inatakiwa ijizatiti kuondoa usumbufu huo.

“Kuna malalmiko mengi kama kuchelewesha mikopo hii, niombe sasa inapotokea hali kama hii taarifa zitolewe kwa wahusika ili wajue changamoto inatokea wapi, ni vyema bodi ikajiwekea commitment (ahadi),” amesema.

Amesema kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya wanafunzi wanasoma kwa kusuasua na kukosa utulivu kwa sababu ya madeni.

Mwakilishi mwingine aliyechangia hoja hiyo ni Haji Shaaban Waziri wa Uzini, ambaye amesema hali za wananchi si nzuri na wapo watu walioshindwa kusoma kwa sababu ya kukosa fedha, lakini kwa kuwa Serikali imeweka mpango huo basi utekelezwe kwa wakati.

“Tuongeze jitihada mikopo hii iwe inakwenda kwa wakati,” amesema.

Huku akishauri wizara iangalie kikwazo kinachochelewesha mikopo hiyo, amesema kiwango cha mikopo kinachotolewa kiongezwe ili isaidie wanafunzi wengi zaidi.

Rukia Omar Ramadhan, Mwakilishi wa Amani amehoji, ikiwa zinatengwa fedha nyingi kwa ajili ya mikopo, kitu gani kinakwamisha zisipelekwe kwao.

Akichangia hoja hiyo, Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman amesema kuna wanafunzi wanadhalilika kwa sababu ya kukosa fedha wakati mikopo ni stahiki yao.

Mwakilishi huyo amesema mbali ya wale wanaosoma nchini, lakini wapo wanaosoma nje ya nchi, wanapokosa fedha hizo kwa wakati, hujikuta kwenye wakati mgumu zaidi.

Hivyo, amesema kuna haja kwa bodi kutafuta ufumbuzi wa jambo hilo mapema badala ya kuacha usumbufu huu uendelee.

Dk Mohamed ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi mwaka 2023, alikuwa mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe amesema: “Tunayasema haya kwa sababu sisi wengine tumeyaona mazingira ya wanafunzi vyuoni wanadhalilika hali inakuwa ngumu sana inapoisha mikopo.”

Mbali na kuwapa wanafunzi ‘bumu’ lao, amesema kuna kilio cha muda mrefu cha kutowapandisha madaraja walimu wa vyuo vikuu.

“Huku nako kama hawa hawapandi madaraja, inakuwa ngumu kupata maprofesa na ndiyo maana Zanzibar ina kiwango kidogo cha wasomi wenye elimu hiyo,” amesema na kuongeza:

“Hapa ukitokea mradi wa Benki ya Dunia unaowahitaji maprofesa, Zanzibar tunatoka patupu, hatuna maprofesa, nafasi hizi tutaendelea kuwaachia wengine, hakuna mfumo mzuri wa kupandisha madaraja, Serikali ilitazame hili,” amesema.

Hata hivyo, wakati akihitimisha hoja hiyo, Waziri Lela amesema kuchelewa kwa mikopo hiyo kunatokana Serikali kuchelewa kuiingizia Bodi fedha hizo, lakini wizara imekuwa ikihimiza jambo hilo na linakwenda vyema.

Hata hivyo, amesema pia wawakilishi wahamishe wanafunzi kurejesha mikipo hiyo, ili Serikali ipate uwanda mpana kuendela kuwakopesha wengine.

Amesema licha ya kupangiwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 7,000 hadi mwaka 2025, mpaka sasa wameshawakopesha wanafunzi 7,158.

Awali, akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo, Waziri Lela amesema inakusudia kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 4,877 mwaka 2025/26 na kuongeza makusanyo ya marejesho ya mikopo kutoka Sh5.5 bilioni ya mwaka 2024/25 hadi kufikia Sh5.7 bilioni mwaka 2025/26.

Serikali inalenga pia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopatiwa ufadhili wa SMZ kutoka 75 mwaka 2024/25 hadi kufikia 85 kwa mwaka 2025/26.

Related Posts