Unguja. Pamoja na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya elimu Zanzibar, mazingira magumu wanayoishi walimu yametajwa kuwa kikwazo kwao, yakichangia kushindwa kupata utulivu wa kufundisha shuleni.
Walimu wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za makazi, jambo linalowanyima nafasi ya kuishi maisha yenye hadhi na kutekeleza majukumu yao kwa utulivu.
Wawakilishi wameeleza hayo hayo leo, Jumatatu Mei 26, 2025 katikia wa Baraza la Wawakilishi walipokuwa wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali mjini Ungujai.
Miongoni mwa changamoto walizozitajwa ni pamoja na walimu wengi kutolipwa stahiki zao, licha ya kufanyiwa ugatuzi kati ya mwaka 2019 na 2021.
Akichangia hoja hiyo, Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu amesema yapo malalamiko mengi ya walimu yahusuyo mishahara kutopandishwa.
“Hata posho wanazostahili kulipwa hawazipati, hususan walimu wakuu na wasaidizi wao, hazijalipwa licha ya jambo hili kujadiliwa mara nyingi hapa ndani,” amesema mwakilishi huyo.
Ameiomba Serikali kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), iwajengea walimu nyumba za bei nafuu na kuwawezesha kwa mikopo ya nyumba ili kuwapunguzia adha ya makazi.
Makungu amesisitiza kuwa Serikali ikijenga nyumba za gharama nafuu na kuwakopesha walimu, kutaleta utulivu mkubwa katika ufundishaji.
“Walimu wakiishi kwenye mazingira bora, wanaweza kufundisha kwa utulivu wa akili na kusaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi,” amesisitiza.
Naye Haji Shaaban Waziri, amesema ZSSF ina nafasi kubwa ya kushiriki kwenye ujenzi wa nyumba hizo kwa sababu tayari ina uzoefu wa kujenga nyumba za kibiashara na sasa inaweza kuelekeza nguvu kwenye miradi ya kijamii inayowanufaisha walimu.
Hata hivyo, mwakilishi huyo amepongeza mpango uliopo wa kusomesha walimu zaidi ya 1,039 katika bajeti ya mwaka 2025/26, lakini amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto za msingi za kada hiyo ili kufanikisha malengo ya sekta.
Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa, amesema sekta nyingine zimepandishwa na kupewa posho, lakini kwa walimu, ahadi zimekuwa zikicheleweshwa na kuwakatisha tamaa.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said, aliyesema posho ya Sh150,000 kwa walimu wakuu na Sh70,000 kwa wasaidizi wao haijalipwa kwa muda mrefu na amehoji tatizo liko wapi.
Mussa Foum Mussa wa Kiwani, amesema kama bajeti inaombwa na inapitishwa lakini kwenye utekelezaji kuna kuwa na changamoto, lazima Serikali ije na majibu yanayoeleweka.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema Serikali imefanya uhakiki na imetenga Sh499 milioni kwa ajili ya kulipa posho za walimu wakuu 654 na wasaidizi 757, kuanzia Juni mosi baada ya kukamilisha taratibu za uhakiki.
“Sh282 milioni zimetengwa pia kwa ajili ya kuwalipa walimu waliofanyiwa ugatuzi, fedha ambazo zitaingizwa baada ya taratibu kukamilika,” amesema waziri huyo.
Katika vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inaendelea kutekeleza mpango wa mageuzi katika sekta ya elimu, ikiwemo kuhamasisha uandikishaji wa watoto, kuimarisha nidhamu za wanafunzi na kufuatilia maendeleo yao.
Pia, wizara inapanga kuongeza idadi ya madarasa kwa kujenga shule mpya na za ghorofa, kukarabati madarasa 900, kukamilisha madarasa 300 yaliyoanzishwa na wananchi, pamoja na kuimarisha miundombinu ya vyoo na umeme wa jua katika shule nyingi.
Zaidi ya hapo, Waziri huyo amesema wizara ina mpango wa kuimarisha matumizi ya teknolojia katika shule kwa kutoa vifaa vya Tehama, kompyuta za mezani na mpakato, pamoja na kuendeleza mtalaa mpya wa umahiri kwa elimu ya maandalizi, msingi na sekondari.
“Vilevile, itaendelea kuboresha elimu ya ufundi na amali kwa kujenga vyuo vipya na karakana, na kuzipatia shule vifaa muhimu. Hatua hizi pia zitajumuisha kuimarisha elimu ya juu kwa kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya diploma,” amesema.
Waziri Musa amesisitiza kuwa walimu ni nguzo kuu ya mafanikio ya sekta ya elimu, bila utulivu wao, hata miradi mizuri haiwezi kufanikiwa. “Kwa hiyo tuhakikisha tunatekeleza ahadi kwa wakati ili kuimarisha motisha kwa walimu na tutaboresha kiwango cha elimu Zanzibar,” amesema.