Dar es Salaam. Imani potofu na dhana zisizo sahihi zimekuwa kikwazo kwa maelfu ya Watanzania kutafuta matibabu ya haraka kwa tatizo la mabusha, hali inayoweza kutibika kwa upasuaji rahisi, wataalamu wa afya wameonya.
Mabusha, unaojulikana kwa uvimbe kwenye korodani kutokana na mkusanyiko wa majimaji, ni miongoni mwa magonjwa yaliyopuuzwa katika maeneo ya kitropiki (NTDs) ambayo yamelengwa kutokomezwa duniani. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa takribani wanaume milioni 19.43 duniani wanaugua mabusha.
Licha ya kuwa ugonjwa unaotibika, mabusha bado ni tatizo kubwa la kiafya katika maeneo ambako ugonjwa huu umeenea, hasa kutokana na imani potofu zinazoendelea kushamiri.
Katika baadhi ya jamii za pwani, ugonjwa huu huaminika isivyosahihi kuwa unasababishwa na kunywa maji kutoka kwenye nazi changa. Kwingineko, kuna Imani potofu kwamba ni ishara ya heshima kwa wanaume.
“Imani hizi siyo tu kwamba ni potofu, bali pia ni hatari. Zinawazuia watu kutafuta huduma za matibabu,” amesema Dk Ngwegwe Damas, Mratibu wa Virusi vya Ukimwi (VVU) katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.
Matibabu ya kawaida ya mabusha ni upasuaji wa kuondoa majimaji yaliyo kwenye mifuko inayozunguka korodani.
Hata hivyo, dhana potofu kama vile hofu kuwa upasuaji husababisha ugumba au imani kuwa wanaume wenye mabusha hutoa burudani zaidi kimapenzi kwa sababu ya ‘joto’ linalozalishwa na majimaji hayo huwafanya wengi kuepuka kufanyiwa upasuaji.
Dk Damas ameonya kuwa imani hizi hazipaswi kupuuzwa, hasa pale zinapochochea tabia zinazoongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs).
“Kwa imani hizi, baadhi ya wagonjwa wa mabusha hawaendi hospitali wakihofia kupata ugumba baada ya upasuaji, ilhali baadhi ya wanawake hujitafutia uhusiano wa kingono na wanaume wenye mabusha kwa matarajio ya kupata raha zaidi,” amesema Dk Damas.
Amesisitiza haja ya kuwepo kwa kampeni maalumu za kuelimisha umma ili kubomoa imani hizi potofu na kulinda jamii zilizo hatarini dhidi ya hatari za kiafya zinazoweza kuzuilika.
Athuman Hamis (52), mvuvi kutoka eneo la pwani, ameeleza jinsi alivyoishi na busha kwa miaka mingi, kipindi ambacho anadai alijihusisha na ngono isiyo salama na wanawake wengi waliomwamini kuwa ana mvuto zaidi kutokana na hali yake.
“Nilifanyiwa upasuaji mara mbili. Wa kwanza nilifanyiwa hospitali ya Serikali lakini haukufanikiwa. Baadaye, timu ya madaktari kutoka Ulaya ilikuja na kutoa matibabu bure, na upasuaji huo ndio uliweza kuniponya,” amesema Athuman, ambaye pia alifichua kuwa ni mwathirika wa VVU.
Maofisa wa afya wanaonya kuwa ugonjwa kama huo si wa kipekee na unaakisi mwenendo mpana wa tabia hatarishi zinazosababishwa na upotoshaji wa taarifa.
Dk Akili Kalinga, Mtafiti Mwandamizi wa Afya ya Umma na Mkuu wa Idara ya Afya ya Umma na Uhamasishaji katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), amesema hali hiyo inahitaji hatua za haraka.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Kalinga ameeleza kuwa, mabusha na matende ni magonjwa yanayolemaza na yanasababishwa na Lymphatic Filariasis (LF) na bado hayaripotiwi ipasavyo na hayahudumiwi vizuri katika maeneo mengi ya Tanzania.
Ametaja utafiti wa hivi karibuni wa NIMR katika Wilaya ya Kilwa, wahudumu wa afya ya jamii (CHWs) walitumia teknolojia ya simu za mkononi kuripoti kesi za maradhi ya LF.
Ndani ya mwezi mmoja tu, wahudumu hao walichunguza karibu watu 94,000 na kugundua kesi 1,900 za matende na mabusha.
“Kwa kutumia simu za mkononi, wahudumu wa afya waliweza kutoa taarifa kwa wakati halisi, na madaktari walithibitisha sehemu kubwa ya kesi zilizoripotiwa. Njia hii inaonesha jinsi teknolojia ya kidijitali inaweza kuimarisha ufuatiliaji na mwitikio kwa magonjwa yaliyopuuzwa katika jamii za mbali,” amesema Dk Kalinga.
Amekiri kuwa, ingawa upasuaji bado ndiyo tiba bora kwa mabusha, upatikanaji wa wataalamu waliobobea ni changamoto kubwa katika maeneo ya vijijini.
Dk Kalinga ameongeza kuwa, Serikali iko katika hatua za mwisho za kuandaa mkakati wa kitaifa wa matibabu na usimamizi wa athari za magonjwa yaliyopuuzwa kama mabusha na matende.
“Mpango huu utaimarisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma na kuelekeza juhudi katika maeneo yenye mzigo mkubwa wa magonjwa. Mara utakapoanza kutekelezwa, utakuwa ni mabadiliko makubwa katika namna tunavyoshughulikia magonjwa haya,” amesema.