Unajua madhara kumhamisha mtoto shule?

Dar es Salaam. Wadau wa elimu na wataalamu wa Saikolojia wamesema kumhamisha mtoto kutoka kwenye mfumo mmoja wa elimu kwenda mwingine, kunaweza kumwathiri kitaaluma na kutojiamini.

Imekuwapo tabia ya kuhamisha watoto kutoka shule moja kwenda nyingine, na aghalabu husababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo kufuata mkumbo, mabadiliko ya hali ya kiuchumi, kuhama makazi, kufiwa na wazazi, kupata au kukosa wafadhili wa masomo.

Hali hiyo imechangia kwa baadhi ya watoto wanaohama kujikuta njia panda kwa sababu ya kubadilishiwa mfumo wa elimu waliosoma awali hasa kwa kuzingatia Tanzania ina mifumo miwili inayotumia Kiswahili au Kiingereza.

Grace Ngowi, mkazi wa Kimara mkoani Dar es Salaam, anasema alihamisha mtoto wake wa darasa la tano kutoka shule ya mfumo wa Kiingereza kwenda Kiswahili baada ya kupoteza kazi yake mwaka jana.

“Ilikuwa ngumu kwa mwanangu kuendana na mabadiliko ya mtalaa, alikuwa na wakati mgumu hasa kwa masomo ya hesabu, sayansi na maarifa ya jamii ambayo yameendelea kumtesa hadi sasa kwa sababu ya kutoelewa lugha ya Kiswahili kwa ufasaha,”anasema.

Anasema alijitahidi kuvumilia mtoto wake aendelee kusoma shule ya Kiingereza, lakini ilishindikana na alijikuta ana madeni mengi kwa sababu ya mikopo ya kumlipia ada mtoto wake.

“Kwa sasa namkazania kwenye masomo ya ziada na nimemtafutia mwalimu shuleni kwao ili amfundishe na kwa sasa angalau anaonyesha mwelekeo, kwani ameanza kusogea kwenye nafasi nafuu darasani ambazo zinanipa matumaini kidogo,”anasema.

Naye, Idd Athumani, mkazi wa Temeke anasema baada ya kupata pesa aliwahamisha watoto wake wawili kutoka shule inayotumia lugha ya Kiswahili na kuwapeleka shule ya Kiingereza.

Anasema aliwahamisha wakiwa darasa la tano ingawa walipata shida awali kwani shule ilikuwa ina lugha nyingine tofauti na Kiingereza ilikuwa na lugha ya Kiarabu ambayo ilikuwa ni lazima kusoma.

“Nilivyowatoa shule ya awali walipokuwa wanarudi nyumbani kila siku wanalalamika hawaelewi kwa sababu masomo yote wanajifunza kwa Kiingereza na waliniambia niwarudishe walikotoka, lakini jibu langu lilikuwa moja watasoma nilipowapeleka,”anasema.

Idd anasema japokuwa hawakufanya vizuri darasa la saba, walielewa lugha kwa sababu ya jitihada zake.

Mtaalamu wa saikolojia, Clara Mwambungu anasema mabadiliko ya mfumo wa lugha shuleni, huathiri uwezo wa mtoto kuelewa masomo, hali inayoweza kuathiri utendaji wake kwa muda mrefu.

“Mtoto anapohamishwa kutoka mfumo mmoja wa lugha kwenda mwingine, anakosa mwendelezo wa uelewa wa masomo na hata kujiamini kwake kunapungua. Ni muhimu wazazi kufikiria kwa kina kabla ya kufanya uamuzi huo,” anasema.

Aidha, anasema mtoto anaweza kujikuta akichukia shule kwa sababu ya kutoelewa kinachofundishwa darasani.

Mwalimu Zubeda Ally wa Shule Msingi Mbagala anasema changamoto wanayokutana nayo kwa watoto wanaohamia kutoka kwenye shule za Kiingereza, watoto kujiona kama wakosefu na kuishi kwa kujitenga kwa sababu ya kutoelewa masomo.

“Nina uzoefu wa kukutana na wanafunzi waliotoka kwa wenzetu, ukikaa nao wanasema hawaewi darasani na kwa namna shule zetu zilivyo na wanafunzi wengi, wanahisi kama wameonewa kuletwa huku,”anasema.

Anasema ili kumsaidia mtoto wa aina hiyo, hujipa muda wa kuzoeana naye na kumuweka karibu, huku akishirikisha baadhi ya walimu kwani wakielekezwa vizuri wanafanya vizuri japokuwa sio kwa kiwango kikubwa.

 “Wanakosa maarifa ya msingi ya Kiswahili, na hili huwafanya washindwe kuendana na mada zinazohitaji ufasaha wa lugha. Tunajitahidi kuwasaidia, lakini mara nyingi tunahitaji muda wa ziada wa mafunzo ya lugha,” anaeleza.

Naye, Mwalimu Emmanuel Mushi, anaongeza kuwa wanafunzi kutoka shule za Kiingereza mara nyingi huwa na changamoto ya kukubaliana na mtindo wa ufundishaji wa Kiswahili.

“Mfumo wa Kiingereza mara nyingi unazingatia mbinu za kiutafiti zaidi, lakini mfumo wa Kiswahili unategemea mazoezi na marudio mengi, jambo ambalo linawashangaza watoto wanaohamia,” anasema.

 Mwalimu Diana Nkya kutoka Shule ya St. Anna anasema wanafunzi wanaotoka kwenye shule za Kiswahili hupata changamoto ya kuendana na mazingira ya mfumo wa Kiingereza.

“Wanafunzi hawa mara nyingi wanakutana na msamiati mgumu na istilahi za Kiingereza ambazo hawajazoea. Inachukua muda kuwajengea uwezo wa kuandika na kuzungumza kwa ufasaha, ” anaeleza.

Mwalimu Diana anashauri kuwapo kwa ushirikiano wa karibu kati ya shule za Kiswahili na za Kiingereza, ili kuandaa mwongozo wa pamoja kwa ajili ya wanafunzi wanaohama kwenye hiyo mifumo.

Kwa upande wake, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Jordan Dk Kassim Nihuka, anasema kuna haja ya wazazi kupewa elimu ya kutosha kuhusu kupeleka watoto shule walizo na uwezo nazo hata kama za kulipia zenye ada nafuu, ambazo wanaweza kumudu na si kupeleka shule kwa kufuata mkumbo wa watu.

“Wapo wazazi wanapeleka watoto katika shule za kulipia kwa kufuata mkumbo, hivyo wanapaswa kujiangalia hali zao za uchumi kabla ya kuchukua uamuzi wa kupeleka mtoto kwenye shule hizo,”anasema.

Aidha, anashauri wazazi kuwa karibu na watoto wao pindi wanapowahamisha shule ili kujua maendeleo yao na kujaribu kuwatafutia walimu wa ziada kwa ajili ya kuwaandaa kwa viwango stahiki.

Related Posts